TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UTEUZI wa Waamuzi sita wa Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi za raundi ya kwanza za All Africa Games zitakazochezwa Aprili 30 mwaka huu na Mei 14 mwaka huu. Waziri Sheha akisaidiwa na Hamis Chang’walu na John Kanyenye atachezesha mechi kati ya Malawi na Afrika Kusini itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu nchini Malawi.
Judith Gamba akisaidiwa na Saada Hussein na Mwanahija Makame atachezesha mechi ya wanawake kwa michuano hiyo kati ya Zimbabwe na Angola. Mechi itafanyika Mei 14 mwaka huu nchini Zimbabwe. Naye Hafidh Ally ameteuliwa kuwa Kamishna wa mchezo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Gabon. DRC ndiyo wenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa Aprili 30 mwaka huu.

U23 v UGANDA


Mechi ya marudiano ya All Africa Games kati ya timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 dhidi ya Uganda itakayofanyika Aprili 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na Athanase Niyongabo kutoka Burundi.

Waamuzi wasaidizi ambao pia watatoka Burundi ni Jean-Marie Hakizimana na Felix Bazubwabo wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ wa Tanzania. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Gaspard Kaijuka kutoka Rwanda.

UCHAGUZI COASTAL UNION, VILLA SQUAD


Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake cha Aprili 13 mwaka huu iliarifiwa kuwa klabu ya Coastal Union ya Tanga inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake hivi karibuni. Ili kufanikisha kikamilifu utekelezaji wa matakwa hayo ya Katiba, Kamati imeitaka Coastal Union kuandaa uchaguzi kwa kuzingatia Katiba ya Klabu inayoendana na Katiba ya mfano ya TFF kwa wanachama wake na pia kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.

Pia Kamati ya Uchaguzi imefuta uchaguzi wa klabu ya Villa Squad ya Dar es Salaam kutokana na kutozingatia kwa utimilifu Kanuni za Uchaguzi. Mchakato wa uchaguzi utaanza tena mara baada ya Villa Squad kukamilisha taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wananachama wa TFF.

NAFASI YA UKOCHA BOTSWANA


Klabu ya Gaborone United Sporting ya Botswana inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo kupitia TFF inasaka kocha mwenye sifa kwa ajili ya kufundisha kikosi chake kwa msimu ujao wa ligi.

Kwa mujibu wa tangazo la nafasi hiyo ya Kocha Mkuu lililotumwa TFF na Ofisa Uhusiano wa klabu hiyo Romeo Benjamin, moja ya sifa hizo ni kuwa na diploma ya ukocha ya chuo/taasisi inayotambulika. Mwisho wa kutuma maombi ni Aprili 30 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari

Post a Comment

0 Comments