TULIWAHI kuandika siku chache zilizopita tukitaka Mwekezaji wa South Beach Hotel ya Kigamboni ashughulikiwe kwa ukatili alioufanya kwa kumuua kijana Lila Hussein kwa moto wa mafuta ya petroli.
Wakati huo wananchi wa Mjimwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam walivamia Hoteli ya South Beach, wakitaka kulipiza kisasi kwa mwekezaji huyo, Salim Noto (53), anayedaiwa kumchoma moto mwenzao, Lila Hussein (25).
Kama ilivyoripotiwa na gazeti hili tena bila kukanushwa na wahusika, kijana huyo alivuliwa nguo na kumwagiwa petroli na mwekezaji wa hoteli hiyo kisha kuchomwa kwa sababu aliingia kwenye ukumbi wa muziki wa hoteli hiyo bila kutoa kiingilio.
Itiliwe maanani kuwa kutokana na kufanyiwa kitendo hicho, mwananchi huyo alijeruhiwa vibaya kuanzia sehemu za shingoni hadi magotini na kulazwa kwa takriban wiki moja kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hata hivyo, kutokana na ukatili mkubwa aliofanyiwa, jitihada za wauguzi na madaktari hazikuweza kuokoa maisha yake na kwa hiyo marehemu alifikwa na mauti usiku wa kumkia Jumapili iliyopita.
Tanzania Daima tunatoa salaam zetu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Lila Hussein. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Awali tulieleza kuwa kitendo kilichoelezwa kufanywa na mwekezaji huyo ni cha ukatili wa hali ya juu na hakikuthamini hata kidogo utu na haki za binadamu; kwamba kinapaswa kukemewa kwa nguvu zote na kuhakikisha kinakomeshwa ili vitendo vya namna hiyo visiendelee kutokea ndani ya nchi yetu.
Hakika haikuwa sahihi hata kidogo kwa mwananchi huyo kuvuliwa nguo na kuchomwa moto, kwa vyovyote vile kilichofanywa ni ukatili kwani hata kama ni kweli mwananchi huyo aliingia kwenye muziki hotelini hapo bila kutoa kiingilio, bado utawala wa hoteli hiyo ungeweza kumkamata na kumchukulia hatua kwa kumfikisha kwenye vyombo vya dola kama polisi na hatimaye mahakamani ambako tuna uhakika asingehukumiwa kuchomwa moto bali angepewa adhabu inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Tukiwa chombo kinachofuatilia haki, fursa, maendeleo na uhai wa watu wa taifa hili, tuliahidi kufuatilia hatma ya sakata hilo kuhakikisha mwekeza huyo anashughulikiwa na moja ya habari za gazeti hili leo imebainisha kuwa mtuhumiwa husika jana alifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Kasimu Mkwawa, na kusomewa shtaka la mauaji.
Tunaunga mkono hatua iliyochukuliwa ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa, tunaamini huko haki itatendeka, lakini hilo pekee bado halitoshi; wakati kesi hiyo ikiendelea, tunaitaka serikali iliyowajibika kumleta mwekezaji huyo ichukue mara moja jukumu la kuhudumia wote waliokuwa wanategemewa na marehemu Lila Hussein mpaka hapo hukumu ya kesi dhidi ya mtuhumiwa aliyemuua au kusababisha kifo chake itakaposomwa.
Mbali na hilo hatutaki kuamini kuwa kitendo hicho alikifanya peke yake, kama kweli alikifanya kama ilivyoelezwa lazima kutakuwa na watu hasa baadhi ya watumishi wa hoteli waliomsaidia au aliowatumia kufanya hivyo. Watuhumiwa wengine akiwemo meneja wa hoteli, Salum Nassoro, na John Mkwanjiombi ambaye ni dereva, waliotajwa kuhusika katika tukio hilo nao wafikishwe mahakamani. Ni wa wajibu wa serikali kukomesha ukatili huu.TAHARIRI HII INAPATIKANA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA TOLEO no. 2387 APRILI 19,2011
1 Comments