Mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam Lila Husein ambaye amechomwa moto na raia wa Kiasia kwa kudhaniwa mwizi katika ufukwe wa Hoteli ya South Beach Kigamboni Dar es Salaam.
Na Hellen Ngoromera
Raia wa Kiasia ambaye ni Mwekezaji wa Hoteli ya South Beach, iliyopo Kigamboni anayefahamika kwa jina maarufu la Chipata anadaiwa kumjeruhi kwa kumchoma moto mkazi wa Mjimwema, Lila Hussein (25) baada kuingia hotelini hapo bila kulipa kiingilio.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, ndugu wa majeruhi huyo, Abdullah Saiwaad,alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi majira kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku. Alisema kabla ya kuchomwa moto, Lila ambaye amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Temeke akiwa hajitambui, alivuliwa nguo kisha kumwagiwa mafuta ya petroli na kwamba amejeruhiwa vibaya kuanzia sehemu za magotini hadi shingoni. Alisema chanzo cha tukio hilo ni Lila kuingia kwenye muziki hotelini hapo bila kulipa kiingilio.
“Hali ni tete, Lila yupo hospitali ya Temeke akipigania maisha yake baada ya kuchomwa moto na mhindi ambaye ni mmiliki wa hoteli ya South Beach, ameungua vibaya tunamwomba Mungu anusuru maisha yake,” alisema Saiwaad. Alisema baadaye aliokolewa na wafanyakazi wawili baada ya kuamua kupeleka taarifa kijijini Mjimwema.
Kutokana na tukio hilo wanakijiji wametishia kuchoma moto hoteli hiyo na kwamba hali hiyo imesababisha mkuu wa kituo cha Kigamboni kupeleka askari wa doria kusimamia usalama hotelini hapo. Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kuahidi kuzifuatilia kwa kina. Kwa mujibu wa Misime, usiku askari walipata taarifa kuwa kuna mtu amechomwa moto hotelini hapo ndipo walipokwenda na kumchukua majeruhi na kumpeleka katika kituo cha afya Kigamboni kisha baadaye kupelekwa Temeke.
Hata hivyo, habari zinapasha zaidi kwamba baadaye jioni ya jana, Lila alihamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) kutokana na hali yake kuwa mbaya.
0 Comments