CHADEMA WATOA RAMBIRAMBI KWA UBALOZI WA JAPAN

Mwenyekiti wa CHADEMA (MB) Freeman Mbowe akikabidhi kiasi cha Dola 2000 za Kimarekani kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania Hiroshi Nakagawa



Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mchango wa dola elfu mbili Ubalozi wa Japan kwa ajili ya maafa
Taarifa inatolewa kwa umma kwamba leo tarehe 23 Machi 2011 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) kimewasilisha mchango wa dola elfu mbili kwa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kwa ajili ya maafa na kutoa salamu za rambirambi kutokana na majanga yaliyoikumba nchi hiyo na watu wake katika siku za karibuni.
Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe (Mb) ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alitumia nafasi hiyo kumweleza balozi wa Japan nchini Tanzania Hiroshi Nakagawa kuwa viongozi na wanachama wa CHADEMA wako pamoja na serikali ya nchi na watu wake katika kipindi hiki kigumu.
“ Mchango wetu wa rambirambi ya dola elfu mbili kwa ajili ya maafa, ni kiasi kidogo kutoa kwa taifa ambalo limekuwa likiisadia nchi yetu na wake kwa kiwango kikubwa; hata hivyo ni ishara ya upendo na ushirikiano wa hali na mali tukiwatakia heri katika jitihada zenu za kukabiliana na maafa yaliyotokea ”, alisema Mbowe.
Akipokea rambirambi hizo Balozi Nakagawa amesema kwamba mchango huo na mingine ya kimataifa inawapa moyo wananchi wa nchi hiyo, hivyo pamoja na kuwa maafa yaliyotokea ni makubwa yaliyosababisha hali ngumu taifa hilo litaendelea kukabiliana na hali hiyo. Alisema kwamba pamoja na tathmini ya madhara kuendelea lakini mpaka sasa inakadiriwa kwamba nchi hiyo imepata athari ya zaidi ya dola bilioni 300.
Katika msafara huyo Mwenyekiti Mbowe aliambatana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje (CHADEMA) John Mnyika (Mb) ambaye pia ni katibu wa wabunge wa CHADEMA, Mjumbe wa Kamati Kuu Hezekieh Wenje (Mb) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Mjumbe wa Kamati Kuu Tundu Lissu (Mb) ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani na wabunge wa Viti Maalum Mhonga Said na Joyce Munkya.
Katika msafara huo viongozi hao walisaini daftari la maombolezo na kukabidhi kadi ya salamu za rambirambi na shada la maua kwa balozi husika.
Katika ujumbe wake kwenye daftari la maombolezo Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, John Mnyika ameeleza kuguswa na utulivu na uvumilivu wa wananchi wa Japan katika kipindi cha maafa na kueleza matarajio yake kwamba taifa hilo litaweza kukabiliana na matokeo ya majanga hayo.
Tukio hilo la Mwenyekiti Mbowe kuwasilisha rambirambi ubalozini na utekelezaji wa azimio la Kamati Kuu ya CHADEMA iliyofanyika tarehe 19 Machi 2011. Kamati Kuu ilieleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya janga la tsunami iliyotokea Japan ambayo nayo imesababisha milipuko wa mitambo ya nyukilia, ambayo kwa pamoja yamesababisha maafa makubwa ya kibinadamu na mali nchini Japan. Kamati Kuu iliazimia kutoa salamu za rambirambi na pole kwa Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Naoto Kan na wananchi wa nchi hiyo.Kamati Kuu iliagiza Sekretariat ya Kamati Kuu kuangalia uwezekano wa kutoa msaada wowote kusaidia ndugu zetu wa Japan ambao wameathirika na maafa hayo.

“Kutoa ni moyo na si utajiri na chochote hicho kiwasilishwe na uongozi wa Chama kwa Ubalozi wa Japan haraka iwezekanavyo kama ishara ya wanachadema, wapenzi na wananchi kwa ujumla kushirikiana na ndugu zetu wa Japan ambao kwa muda mrefu wamejitolea kwa hali na mali katika kusaidiana na Watanzania katika maendeleo na majanga mbalimbali”, lilisema azimio hilo la Kamati Kuu.

Imetolewa na:

Erasto Tumbo
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Post a Comment

0 Comments