Bendi ya Muziki wa dansi ya The African Stars ‘Twanga International’ wanaotamba kwa mtindo wa Sugua Kisigino inatarajiwa kuuaga mwaka kwa staili ya kimataifa, imefahamika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam , Kiongozi wa bendi hiyo, Luiza Mbutu alisema, katika mkesha wa kuaga na kuukaribisha mwaka mpya, watakuwa hoteli ya Safari Park jijini Nairobi Kenya.
Aidha, Luiza alisema kuwa onyesho hilo linalokwenda kwa jina la ‘Dinner & Dance’ kiingilio chake kitakuwa dola 100 za Marekani kwa mtu mmoja.
Wakati huo huo, Mbutu alisisitiza kuwa baada ya kuukaribisha mwaka Twanga Pepeta watakwenda katika tamasha la Kimataifa la muziki katika Falme za Kiarabu, Muscat Oman.
“Huu ni mwanzo tu wa bendi yetu isiyo na mpinzani nchini, Mungu akipenda mwakani tutazuru katika nchi nyingi ili kujitangaza zaidi kimataifa ,” alisema Mbutu.
Hivi sasa bendi hiyo inajiwinda na albamu yake ya 11, ikiwa tayari imeachia ngoma mbili gumzo jijini ambazo ni ‘Mapenzi Hayana Kiapo’ na ‘Kauli’ .
0 Comments