Miss utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga (kushoto) akiingia
kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam jana, kuelekea Equatorial Guinea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano
ya Dunia ya Miss Tourisim World 2013, pembeni ni mshindi wa tatu, Teresia
Kimolo. aliyemsindikiza (Picha na Hosea Joseph)
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limempa karipio kali
Mwenyekiti wa shindano la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo kwa kosa la
kudhalilisha baadhi ya washiriki na malalamiko kufanyiwa kazi na Baraza hilo .
Karipio hilo
lilitolewa baada ya Basata kupitia tathmini iliyohusisha vipande vya matukio
yaliyorekodiwa (clips) na kujionea namna wasichana wanavyofanyiwa vitendo vya
udhalilishaji na Chipungahelo kwa kipindi cha kambi ya miezi mitatu.
Katika hafla ya upitiaji wa clips hizo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Basata,
Ilala, jijini Dar es Salaam mbele ya Chipungahelo, ilionekana wazi
wasichana kukosa uangalizi walipokuwa kambini, hivyo kuwepo kwa matukio
mbalimbali yasiyofaa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa kitengo cha Sanaa wa
Basata, Nsao Shaluwa alisema baada ya kupata malalamiko kuwa wasichana
wanafanyiwa mambo yasiyofaa wakiwa kambini, waliamua kuutafuta ukweli na
kujiridhisha shindano hilo
lina ukakasi mwingi.
Alisema baada ya kukusanya baadhi ya matukio katika
kuthibitisha hali halisi iliyopo kwenye shindano hilo ,
watapeleka vielelezo kwa Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana Michezo na
Utamaduni ili Chipungahelo ajadiliwe kwa kosa la kudhalilisha warembo wa
shindano hilo .
Alisema kwa kukosa matroni, yaelezwa warembo walikuwa wakizurula kutwa nzima hadi usiku kwenye gari
huku kukiwa hakuna ratiba ya chakula ya kueleweka huku wakifanyishwa mazoezi
muda mrefu.
Mbali ya muda mrefu kuanzia saa 2 usiku hadi 9, pia walikuwa
wakivaa viatu virefu, hivyo miguu kuvimba na wakati mwingine walikuwa
wakichapwa makofi na kulazimishwa mapenzi.
Aidha, Chipungahelo anakabiliwa na shutuma ya kuwaweka
mabini washiriki kwa muda wa miezi mitatu tofauti na alivyoeleza Basata kuwa
kambi ni ya wiki tatu.
Zaidi ya hapo, Chipungahelo alishindwa kutoa zawadi kwa
washindi wala kifuta jasho kwa washiriki wengine huku mshindi wa mwaka 2013,
akidaiwa kubebwa kwa hila.
Shaluwa alisema baada ya malalamiko hayo kufikishwa kwao,
waliamua kunyatia katika kambi yake
iliyokuwa na warembo saba ambayo pia Chipungahelo aliwaficha.
Baada ya kuwahoji washiriki, walikiri kwamba walikuwa
wakilala warembo saba, wengine watano katika chumba kimoja na wengine wakilala
chini huku wakila mlo mmoja tena katika muda usiofaa.
“Warembo wengi
wamekiri walikuwa wakifanyishwa mazoezi
kwa muda mrefu huku wakiwa wamevaa viatu virefu,
“Tulikuwa tukifanyishwa mazoezi kuanzia saa mbili usiku hadi
saa tisa, tuna njaa na tulipolalamika, baba alitutukana matuzi ya nguoni na
kukashifu tupu zetu” mmoja wsa warembo alisema katika CD ya Basata.
Shaluwa anasema walipofika Ikondolelo ambako kulikuwa na
kambi ya awali, walizungumza na warembo
hao, lakini wakishindwa kusema ukweli mbele ya Chipungahelo.
Alisema walipowapa karatasi kuandika kero zao, kila mtu
aliandika jina na kusaini ambapo walieleza mengi yaliyorekodiwa na wadau
kuoneshwa mwishoni mwa wiki mbele ya mwanasheria Ashura Mzava kutoka TAWLA.
Mzava alisema wazi
kwa madudu yaliyopo kwenye shindano hilo , Chipungahelo anapaswa kushtakiwa kwa
udhalilishaji.
Kashfa nyingine ni kitendo cha Chipungahelo kutumia kiasi
cha sh 200,000 ambazo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya Tanga Mjini, Halima Dendego ili washiriki
waende saloon kabla ya fainali.
“Baba ametunyanyasa sana
hadi, ametumia pesa tuliyopewa na mama Halima Dendego, lakini hapohapo amekuwa akimpendelea mshiriki
mwenzetu (jina tunalo), kwa vile alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi,”
alisema mmoja wa washiriki na kuongeza:
“Hata siku ile ya fainali, alipokuja mpambaji kutoka Sofia
Record, alimuita na kumvalisha nguo nzuri pamoja na kumpamba tofauti na
alivyovalisha washiriki wengine”
wamesema washiriki hao.
Wakati huohuo Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa kutoka Wizarani, Leah Kihimbi alisema
atalifikisha kwa usahihi suala hilo katika ngazi ya
juu akimtaka Chipungahelo ajitayarishe
kwa maamuzi yoyote.
Mshiriki pekee wa Miss Utalii 2013 aliyefika kwenye tahmini hiyo, ni Glory John aliyesema
wazi shutuma zote zilizoelezwa na wenzake dhidi ya Cipungahelo ni kweli.
“Tulipokuwa
tunakwenda Mikumi , tulilala Morogoro, Baba (Chipungahelo) aliniita akaniambia
nipande juu katika chumba kimojawapo, nilipokwenda na kufungua mlango,
nikakutana na moshi wa ajabu nikashindwa kuvumilia nikatoka.
Akanifuata akinitaka nirudi chmbani mle, nikagoma,
nilipowaeleza wenzangu, walinieleza nilielekea kunaswa kwenye mtego wake,”
alisema Glory.
Naye Katibu Mtendaji
BASATA Godfrey Mngereza alisema, hilo ni suala nyeti
linalogusa jinsia ya kike, hivyo ni
hatari kwa ustawi wa jamii.
Kupitia tathmini hiyo ya aina yake, Basata itachunguza
mazingira ya ushindi wa Miss Utalii mwaka 2013, ikibainika hakustahili,
atavuliwa taji hilo
ili iwe fundisho.
“Tabia hizi chafu zinatuchafua hata sisi BASATA tunaonekana
hatufanyi kazi sasa ndio tutaanza na Miss Utalii na ikibidi kusiwe na shindano
la aina yeyote kama mambo yenyewe ni
kudhalilishana,” alisema Mngereza.
Wadau wengine
waliohudhuria tathmini hiyo ni
kutoka TAMWA, TAWLA,TGNP,THAWE, Polisi Jamii, Polisi kutoka kituo cha Pangani
Ilala, Dar es Salaam, Shirikisho la Sanaa
na Ufundi, Binti Leo na wengineo.
Shaluwa alisema suala hilo
litapelekwa ngazi za juu na vielelezo kuonesha wasichana wakieleza yanayotokea
kambini pamoja na maoni ya wadau yaliyorekodiwa.
Akizungumnzia tuhuma dhidi yake, Chipungahelo alisema ni
majungu yaliyopikwa na maadui zake ambao walimpandikizia makahaba kwa lengo la
kuchafua taswira ya shindano
hilo ili kummaliza, lakini aliomba radhi kwa dosari na
mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kuwa hazitajirudia tena.
0 Comments