Taasisi ya Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika ijulikanayo kama Africa Bee Expo, imeialika Tanzania kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Tano ya Ufugaji wa Nyuki Afrika yatakayofanyika mwaka 2028 na kujumuisha wafugaji wa nyuki kutoka takribani nchi 50.
Mualiko huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bw. Fatah Ben Chouia wa Algeria, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Algiers.
Pamoja na mwaliko huo, Bw. Chouia aliwasilisha pia mwaliko wa Tanzania kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Nne ya Ufugaji wa Nyuki Afrika yatakayofanyika jijini Algiers, Algeria, tarehe 3-6 Septemba, 2026, na kuziomba taasisi za serikali na watu binafsi wa Tanzania kushiriki.
Balozi Matinyi aliishukuru taasisi hiyo kwa kuipa Tanzania heshima ya ugeni rasmi mwaka 2026 na uenyeji mwaka 2028 na kuahidi kwamba Serikali itaifanyia kazi mialiko hiyo kwa manufaa ya sekta hiyo ambayo hutoa fursa ya ajira milioni mbili kwa Watanzania na kuchangia katika pato la taifa.
Bw. Chouia aliipongeza Tanzania kwa kuwa moja ya nchi zenye mafanikio makubwa katika ufugaji wa nyuki na mazao yake barani Afrika na duniani kiasi cha kustahili kuwa mwenyeji wa maonesho hayo barani Afrika kwa mwaka 2028.
Maonesho ya nyuki na mazao yake barani Afrika hujumuisha pia nchi zingine duniani kote na hutoa fursa ya kukutanisha wajasiriamali, wataalamu na watafiti wa ufugaji wa nyuki katika kongamano la kimataifa la utaalamu wa ufugaji wa nyuki, uhifadhi na uzalishaji wa bidhaa zake.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji Nyuki (Apimondia), Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika na ya kumi duniani kwa uzalishaji asali unaofikia tani 31,000 na pia tani 1,800 za nta kwa mwaka.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Juni 3, 2026.

0 Comments