SKA 2026 KUCHOCHEA UANDISHI WA HABARI ZA MAENDELEO

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) zimeanza maandalizi ya Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 zikiwa na lengo la kuendelea kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yenye ubora yanayochangia maendeleo ya Taifa.

Akizungumza Jumapili tarehe 31 Mei, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Mwenyekiti wa SKA, Mha. Peter Mwasalyanda, amesema SKA ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kutambua mchango wa Waandishi wa Habari za maendeleo nchini.

Amesema tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, huku yakiimarisha taswira chanya ya Taifa kupitia habari za maendeleo. 

Mwasalyanda amesema katika awamu ya kwanza ya tuzo hizo kulikuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya habari wakiwemo taasisi za habari, Waandishi wa Habari binafsi, watengenezaji wa maudhui mtandaoni na Maafisa Habari wa Serikali. 

Amesema kabla ya mashindano hayo, mwaka jana TCRA na TAMWA waliendesha mafunzo maalumu yaliyowanufaisha zaidi ya Waandishi wa Habari 2,000, hatua iliyochangia ongezeko la maudhui ya ndani yenye ubora na tija kwa jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMWA, Dkt. Kannaeli Kaale, amesisitiza umuhimu wa Waandishi wa Habari kutumia tuzo hizo kama jukwaa la kuibua na kusimulia mafanikio ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili wananchi na dunia kwa ujumla ziweze kutambua hatua zinazopigwa.

“Nasisitiza waandishi wa habari kushiriki kuwania Tuzo za Habari za Maendeleo za Samia Kalamu Awards 2026, kwa kuwa waandishi wa habari ndio daraja kati ya serikali na wananchi, tuendelee kuandika habari za miradi ya maendeleo, tuone umuhimu wa kusemea miradi yetu hatua tunazopiga za kimaendeleo. Naomba muachane na maneno kwamba kushiriki tuzo hizi ni kwamba umenunuliwa, siyo kweli.” amesema Dkt. Kaale.

Aidha, Mwasalyanda amesema ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na ushindani wa haki, maandalizi ya tuzo hizo yanahusisha pia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amewahimiza Waandishi wa Habari wenye ithibati kushiriki kwa wingi katika mashindano hayo, akisisitiza kuwa mwaka huu ithibati ni miongoni mwa vigezo vya ushiriki. 

“Mtakumbuka Msimu wa kwanza wa Samia Kalamu mambo ya JAB hayakuwepo, kwa hiyo waandishi walishiriki wote bila kujali vigezo vya Ithibati lakini mwaka huu kuna hiki kigezo cha kuwa na ithibati kwa hiyo niwashauri basi wote wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati, wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.” Amesema Wakili Kipangula na kuongeza;

“Ni muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isije ikaonekana ni tuzo za watu fulani tu, kila mmoja awasilishe habari hasa zile ambazo zimezingatia maadili, zimezingatia weledi, lakini pia habari ambazo zina impact kwa kwa wananchi,” amesema Kipangula.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mchakato wa kupokea kazi umeanza rasmi Mei 31 na utafungwa Juni 30, 2026 kupitia tovuti ya samiaawards.tz, huku tuzo hizo zikitarajiwa kutolewa kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments