Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuwapuuza wanaodai kuwa watawasindikiza wanatakao kwenda kupiga kura ya mapema 28 Oktoba 2025.
Kikatiba siku moja kabla ya kupiga kura wananchi wote, vyombo vya ulinzi na usalama ndio wanaoenda kupiga kura ili siku inayofuata wabakie na majukumu yao ya ulinzi na usalama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Bumbwini katika uwanja wa mpira Vidimni, wilaya ya Kaskazini 'B', Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema kuna watu amewasikia wakisema hivyo kauli ambayo ina mwelekeo wa uvunjifu wa amani.
"Kuna watu nawasikia wanasema 28 Oktoba watatoka kuwasindikiza, wanaoenda kupiga kura, mimi nawaambia msitoke, acheni waende wao kama hodari" alisema.
Alisema msingi wa CCM ni amani na maendeleo yanayoonekana katika sekta ya afya, miundombinu, elimu ni kutokana na kuwepo amani.

0 Comments