CCM: DEMOKRASIA SIYO KUGAWANA MADARAKA

Mwandishi Wetu , Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema siku ikitokea kikashindwa Uchaguzi Mkuu kwa matakwa ya kura za wananchi hakitasita kukubali matokeo lakini siyo kugawa madaraka kama hisani kwa chama chochote cha siasa.

Akizungumza, Mjini Unguja,tarehe  06 Oktoba 2025 kufuatia hoja ya ACT Wazalendo ya kutaka kugawana madaraka, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC za Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis alisema madaraka hayatolewi kwa hisani, huruma wala ushemeji isipokuwa ni chama kukubalika kwa umma.

Mbeto alisema CCM kimesistiza upinzani wa Zanzibar haujapevuka na kuwa madhubuti kiasi cha kuwaridhisha wananchi ushike madaraka.

Chama hicho Mbeto alisema, mgombea wa nafasi ya Rais Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman atambue kuwa bado watu hawakijakiamini chama chao kwa itikadi na kukosa sera nae kubaki na misimamo yake na aina ya viongozi walionao ili kipigiwe kura za kushika utawala.

Alisema Wananchi hususan wa Zanzibar ni wakomavu kisiasa, werevu wanaopima mambo bila kukurupuka hivyo hawajapata sababu ya kukiacha CCM na kuuchagua upinzani.

'Upinzani bado una kazi ya kujitafakari. Lazima wajue kwanini wananchi wanawakataa, matamshi yao hayaonyeshi kujali umoja, wananadi ubaguzi mambo ambayo hayakubaliki popote" alisema Mbeto 


Katibu Mwenezi huyo alisema kujenga taasisi ya kisiasa imara inayoaminiwa na wananchi, si jambo la muda mfupi, badala yake ni mchakato unaohitaji kupata sera mbadala , hoja yakinifu na dira sahihi.


"ASP toka mwaka 1957 kimevibwaga vyama vya ZNP na ZPPP na ilitokea hivyo havikutokana na matakwa ya wengi. Wananchi wote waliunga mkono sera za ASP na wagombea wake" alibainisha na kuongeza kuwa ACT inatakiwa ijifunze kupitia historia.


Mbeto alisema kizazi cha sasa kuelekea miaka hamsini ijayo,ni kile kilichotokana na Mapinduzi  

ya Zanzibar mwaka 1964 ambayo ndiyo yaliovunja matabaka na utawala uliodumu miaka takribani 104 iliyopita.


"Makundi ya wananachi wa kizazi hiki wamesomeshwa kwa chini ya sera za CCM ambazo zimerithiwa toka TANU na ASP chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambazo zimekomesha ubaguzi, upendeleo na kuwajali wanyonge na masikini " alisema. 

Alisema wanapotokea wanasiasa wa upinzani kuanza kuhubiri sera zisizoijengea matumaini kwa jamii wana haki ya kuvikataa vyama hivyo . 

"Mgombea anaposema utatoa nchi taka usitake huyo ameshabaini atashindwa ndio maana anatumia lugha ya vitisho" alisema Mbeto.

Post a Comment

0 Comments