Na Mwandishi Wetu, Pemba
Jumla ya wanachama 364 wa Chama cha ACT-Wazalendo wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) na kula kiapo cha utii huku wakimkabidhi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kadi zao za kama ishara ya kuiunga mkono CCM na mgombea nafasi ya Rais Zanzibar Dkt. Mwinyi.
Wanachama hao wamejiunga na CCM katika mkutano wa hadhara wa kampeni za chama uliofanyika 06 Oktoba 2025
Uwanja wa Michezo wa Msuka, Jimbo la Konde, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mgombea huyo wa CCM aliwakaribisha wanachama hao na awali alisema, wananchi wana wajibu wa kuhakikisha amani inadumu, kwani ndiyo msingi wa maendeleo yote, na ameahidi kuisimamia iliyopo.
Dkt. Mwinyi amesema CCM inajivunia kufanikisha maendeleo Unguja na Pemba yanayotokana maridhiano na kuwaunganisha Wazanzibari.
Amefahamisha kuwa ongezeko la ufaulu wa wanafunzi hivi sasa ni hatua kubwa katika ukuaji wa sekta ya elimu na ameahidi ujenzi zaidi wa shule za kisasa zenye mahitaji yote muhimu.
Alisema katika kipindi kifupi kijacho suala la maji safi na salama litapatiwa suluhisho la kudumu ili wananchi wote wapate huduma hiyo kwa uhakika pamoja na kukamilisha ujenzi wa Bandari ya Wete na ya Shumba, Mjini.
Kuhusu barabara, Dkt. Mwinyi amesema bado ipo kazi ya kufanya, na serikali imejipanga kujenga barabara zote kuu na zile za ndani katika muda mfupi ujao.
Amesema pia serikali katika awamu ijayo itaongeza pensheni kwa wazee na wastaafu, pamoja na kuwawezesha wanawake wanaolima mwani kwa kuwaandalia mazingira bora zaidi, ikiwemo kuwapatia mikopo isiyo na riba na utoaji wa boti kwa wavuvi.
Aidha Serikali inaendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula na itanunua bidhaa kutoka Tanzania Bara wakati wa mavuno, kuhifadhi na kushusha bei kwa wananchi.
Kuhusu zao la karafuu, amesema Serikali imeamua kutoa hati za mashamba ya Serikali kwa wananchi ili wayatunze na kuongeza uzalishaji, na ameahidi Serikali kuendelea kuliimarisha zao hilo tegemeo liendelee kutoa tija kiuchumi kwa Zanzibar.


0 Comments