Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha Leseni ya Maudhui Mtandaoni ya JamiiForums kwa muda wa siku 90 na kuzuia upatikanaji wa jukwaa hilo, kwa maelezo ya kukiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu maudhui mtandaoni
TCRA imesema uamuzi huu umetokana na JamiiForums kuchapisha taarifa ya Mwanasiasa Humphrey Polepole kuhusu Rostam kumiliki mgodi wa makaa ya mawe kwa asilimia 70 na taarifa za uhusiano kati ya Rais wa Tanzania na "Mfanyabiashara" Wicknell Chivayo bila kuzingatia mizania.
Kwa mujibu wa TCRA, JamiiForums ilishindwa kutafuta maoni ya Mamlaka husika/Msemaji wa Rais/Serikali, kuthibitisha uhalisia wa picha (za Rais na Chivayo) zilizotumika, na hivyo kuuaminisha Umma taarifa za upande mmoja.
Aidha, TCRA imeeleza kuwa jukwaa la JamiiForums halikudhibiti maudhui yenye lugha ya matusi, kashfa na kejeli dhidi ya Rais wa Tanzania, na kuendelea kuhifadhi maudhui hayo ambayo bado yanapatikana kwa umma.
TCRA imeongeza kuwa maudhui hayo yanakinzana na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania, hivyo kuhatarisha mshikamano wa kitaifa, amani na taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

0 Comments