CCM: DKT. HUSSEIN MWINYI ANASTAHILI KURA NYINGI MICHEWENI

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Wananchi wa Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa kumpigia kura mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika uchaguzi mkuu ujao 2025 ili akamilishe miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikutano ya kampeni katika wilaya hiyo, 28 Septemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema Micheweni ndio wilaya iliyopata upendeleo wa pekee katika utekelezaji wa miradi ya kimakakati.

Mbeto alisema wilaya hiyo ina mtandao wa barabara mjini hadi vijijini kuliko wilaya zingine zote Unguja na Pemba sanjari na ujenzi wa bandari ya Shumba Mjini ambayo itafungua mawasiliano baina ya Micheweni na Mji wa Mombasa nchini Kenya.

Alisema ujenzi upo katika hatua tofauti ikiwa ni pamoja na jengo la utawala, gati lipo hatua za mwisho na ujenzi wa banda la kupumzikia abiria.

Viwanda zaidi ya sita vinavyotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni eneo huru la uwekezaji lenye ukubwa wa hekta 800.8 lililo chini ya Kituo cha Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

“Huko tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya kuchakata samaki, vifaa vya umeme na hoteli kubwa za kitalii” alisema na kuongeza kuwa Micheweni hawana sababu za kutokumpa kura za kutosha Dkt. Mwinyi, madiwani na masheha wa CCM.

Mbeto alibainisha kuwa boti 450 zilizotolewa kwa wavuvi na wakulima wa mwani wilayani humo ni sehemu ndogo ya ya mambo makubwa aliyopanga kuyafanya Micheweni.

Mwenezi Mbeto amewataka kuachana na wanasiasa wanaosambaza chuki na utengano kwa waZanzibari badala ya sera za maendeleo kwani siasa za namna hiyo zimepitwa na wakati.

Post a Comment

0 Comments