MAMIA WASHUHUDIA UZINDUZI WA SAMIA LEGAL AID PWANI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akizungumza kwenye  banda mojawapo kabla ya kuzindua Samia Legal leo tarehe 24 Februari, 2025 .

Kibaha  ,Pwani 

Mamia ya wananchi wa Mkoa wa Pwani wamehudhuria uzinduzi wa Samia Legal Aid na kuifurahia vilivyo huduma hiyo.

Blog hii  imeshuhudia wakaazi hao wakipanga foleni kwenye banda la Huduma ya Vizazi na Vifo RITA ambapo walioonekana kuhitaji huduma ni watu ambao hawana vyeti vya kuzaliwa licha ya umri mkubwa waliokuwa nao.

Akizindua huduma hiyo  ya Samia Legal Aid. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakar Kunenge ametoa wito kwa Wanasheria Mkoani hapa  kuwahudumia wananchi kwenye kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

RC Kunenge amesema hayo leo tarehe 24 Februari Mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo ambapo huduma hiyo itatolewa  kwa  siku tisa ndani ya Mkoa wa Pwani.

 "Nawasihi wananchi wa Pwani jitokezeni kwa wingi  kuleta kero zenu kwa wataalamu wa sheria kwa sababu  itawasaidia wananchi wanyonge ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za kisheria" amesema Kunenge. 

 "Nashkuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kubuni kampeni hii ambayo italeta faraja na kurudisha  matumaini kwa wananchi ambao ni wanyonge" amesema Kunenge.

 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amesema kuwa Kampeni hii itaanza kesho Februari  25 hadi Machi 5 mwaka huu huku ikiwa na lengo la  kuwezesha wanyonge wanapata haki zao kwa wakati.

Naye Naibu Waziri wa maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Mwanaidi Khamis amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia, matunzo ya watoto, ardhi na ubakaji yamekithiri huku amewataka wananchi kutumia fursa ya huduma hii ya msaada wa kisheria  iliyowafikia na kusisitiza  kuwa Mhe.Rais Dkt.Samia amelenga kuwarejeshea wananchi tabasamu kwa kupata haki zao ambazo wamekua wakishindwa kuzipigania kwa kukosa ufahamu juu ya Sheria husika hasa kwenye masuala ya ndoa,mirathi,
ardhi   na haki ya matunzo kwa mtoto.

Aidha Mwakilishi  wa Bodi ya Ushauri wa msaada wa Kisheria Nuru Awadh amesema kuwa siku tisa ni chache kwani changamoto ya masuala ya kisheria ni kubwa sana hivyo ili kuwafikia wananchi wengi amemuomba Mkuu wa Mkoa  wa Pwani  kuwe na dawati ambalo litakuwa linatoa  huduma hii na kuwaendelevu.

Mkurugenzi wa Mashirika yanayotoa msaada wa kisheria (TANLAP) Christina Ruhinda amesema kuwa kila Kata ina wasaidizi wa kisheria nchi nzima ambao kazi yao ni kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu  na msaada wa kisheria.
Baadhi ya waananchi wa Mkoa wa Pwani waliojitokeza kwenye uzinduzi wa Kampeni hiyo ya Samia Legal Aid.
Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria Jumanne Sagini. 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashidi Mchatta.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akisisistiza jambo kwenye uzinduzi wa Samia Legal Aid  uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya zamani Mailimoja Kibaha. 
Wakati huohuo 
Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa, ameiomba  Serikali  kutoa elimu kwa wanandoa wa dini ya Kiislamu kusajili vyeti vyao vya ndoa na kuweza    kutambulika kisheria tofauti na ilivyo hivi sasa kwani  havitambuliki.
Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), cheti cha ndoa cha dini hakitoshi kukutambulisha kama mke na mume inapofika kwenye masuala ya kisheria pindi watu waapoachana ama mirathi jambo ambalo hupoteza haki kwa wahusika  ama muhusika anapidai stahiki zake kisheria pindi shauri linapofikishwa Mahakamani. 

 Sheikh Mtupa amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya  Samia Legal Aid.

Mtupa amesisitiza kwa kusema  kuwa cheti hicho kinatambulika na
BAKWATA tu  jambo ambalo linazua usumbufu kwa waumini wa dini hiyo. 

“Ili ndoa itambulike kisheria, lazima isajiliwe na Wakala wa Serikali na kupewa cheti cha ndoa cha Serikali,” amesema Mtupa.
Kampeni hii tayari imefanyika kwenye mikoa 19 huku Pwani unakua  Mkoa wa 20.

Wizara ya Katiba na Sheria  imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo Mei, 2025, kampeni itakuwa imetekelezwa kikamilifu katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments