MTAMBI AONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MEJA JENERALI MBUGE

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amewaongoza viongozi, wananchi na waombolezaji katika mazishi ya Meja Jenerali Mstaafu Charles Mang’ere Mbuge aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Idara ya Majanga na Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu. 
Akizungumza katika mazishi hayo, Mhe. Mtambi ametoa pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na waombolezaji wote na kuwataka waombolezaji hao kutafakari kuhusu safari yao ya maisha hapa duniani. 
“Maisha ni siku tatu: jana, leo na kesho, jana huijui leo tunayo, kesho huijui, kumbe sote tutaenda njia hii aliyotangulia mwenzetu na suala la msingi la kujiuliza tunaendaje? Mwenzetu kaenda vizuri, sisi tutaendaje?” amesema Mhe. Mtambi. 
Mhe. Mtambi amesema kwa kawaida watu huwa wanafariki mwezi mmoja kabla, mwezi waliozaliwa au mwezi mmoja baada ya mwezi wa kuzaliwa na Meja Jenerali Mbuge alizaliwa tarehe 06 Oktoba, 1963 na amefariki tarehe 12 Oktoba, 2024. 
“Ni imani yangu kuwa wakati wake ulikuwa umefika na amepumzika, na amepumzika kupumzika ambako wengine tunasema kumetukuka…. Amepumzika vizuri kweli kweli kazi kwetu sisi ambao bado tuna uhai tujitafakari maisha yetu” amesema Mhe. Mtambi. 
Akizungumza katika mazishi hayo, Mhe. Mtambi amesema marehemu kama wazungumzaji wengi walivyosema alikuwa mchapakazi sana kama ilivyo sifa ya wananchi wa Mkoa wa Mara na kuongeza kuwa wanamara ni wachapakazi sana. 
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wa Kanda ya Ziwa Mhe. Mtambi amesema marehemu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, moja ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na katika mazishi hayo kuna uwakilishi kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na wanayo rambirambi yao ambayo wataiwasilisha kwenye familia ya marehemu. 
 Nyamongo, Kata ya Kukilango Tarafa ya Makongoro, Wilaya ya Butiama na amefariki tarehe 12 Oktoba, 2024 katika Hospitali ya Appolo nchini India na baadaye kurudishwa nchini tarehe 14 Oktoba, 2024. 
Mhe. Mtambi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi na waombolezaji kujiandikisha katika daftari la mkaazi wa Mtaa/Kijiji zoezi linaloendelea kitaifa hadi tarehe 20 Oktoba, 2024 ili waweze kushiriki kupiga kuwa katika uchaguzi Serikali za Mitaa utakaofanyika hapa nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Taarifa ya wasifu wa marehemu inaonyesha kuwa alizaliwa tarehe 06 Oktoba, 2024 katika Kijiji cha Nyamongo.
Meja Jenerali Mbuge amesoma Shule ya Msingi Lugalo mwaka 1974-1980 na Shule ya Sekondari Kigurunyembe mwaka 1981-1984 na baadaye akajiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tarehe 01 Januari, 1985 na amelitumikia jeshi kwa muda wa miaka 38, miezi saba na siku nne.  
Mhe. Mbuge alihudhuria kozi mbalimbali ikiwemo kozi ya Afisa Mwanafunzi nchini Tanznaia na kutunukiwa Kamisheni tarehe 28 Machi, 1991 na alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali hadi cheo cha Meja Jenerali tarehe 02 Juni, 2020. 
Meja Jenerali Mstaafu Mbuge amewahi kushika madaraka mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 2019-2021, Mkuu wa Mkoa wa Kagera mwaka 2021-2022 na Mratibu wa Idara ya Majanga na Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2022 hadi alipostaafu jeshini kwa heshima tarehe 05 Oktoba, 2023. 
Viongozi na waombolezaji mbalimbali waliopata nafasi ya kutoa salamu wamemzungumzia Meja Jenerali Mstaafu Mbuge kuwa alikuwa mchapakazi na aliyetekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na muasisi wa neno HAPA KAZI TU!. 
Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mohamed Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenan Kihongosi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mhe. Patrick Chandi Marwa, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Venance Salvatory Mabeyo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini. 
Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Rajabu Mabele, viongozi mbalimbali wa Jeshi, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama, Wakuu wa Wilaya mbalimbali wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Post a Comment

0 Comments