Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi akizungumza wakati wa
mkutano wa wadau kuhusu usalama wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es salaam.
kiongozi wa Timu ya wataalamu wa Afya ya Jamii na Mazingira kutoka Makao Makuu ya Shirika la Afya Duniani,
Geneva, Dk. Ivan Ivanov akizungumza
wakati wa mkutano wa wadau kuhusu usalama wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es
salaam.
Na Aron Msigwa , Dar es Salaam.
Waajiri
kote nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kisheria kwa wafanyakazi
waliowaajiri kwa kuhakikisha kuwa wanaweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi na
kuwapatia vitendea kazi muhimu vya kuwakinga na madhara ya kiafya katika maeneo
yao ya kazi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau kuhusu usalama
wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es salaam, Mganga Mkuu wa Serikali Prof.
Mohammed Bakari Kambi amesema kuwa waajiri wana wajibu huo kwa kuwa maeneo ya
kazi ni sehemu muhimu katika maisha na
uhai wa wafanyakazi kote nchini.
Amesema
watumishi wamekuwa wakitumia muda mwingi kwa siku wakiwa mahali pa kazi kwenye
viwanda, mashamba, maeneo ya kutolea huduma za Afya, migodini na kwenye
shughuli mbalimbali hivyo mazingira hayo lazima yawe salama kwa afya zao.
Ameongeza
kuwa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini karibu kila siku wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zenye athari kwa afya zao hasa athari za
kibiolojia, Kemikali, ajari za viungo vya miili yao, matatizo ya usikivu yanayotokana
na mazingira yenye kelele na changamoto mbalimbali ambazo wakati mwingine
husababisha vifo.
“Wapo
baadhi ya waajiri hawatimizi wajibu wao wa kisheria wa kuhakikisha wanalinda
afya za watumishi wao kwa kuwawekea mazingira safi na salama, jambo hili halikubaliki”
Amesisitiza Prof. Mohammed.
Amesema
Serikali kupitia wizara ya Afya ikishirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya
Afya itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi katika sehemu zao
za kazi kazi ili kulinda afya zao.
Kwa
upande wake kiongozi wa Timu ya wataalamu wa Afya ya Jamii na Mazingira
kutoka Makao Makuu ya Shirika la Afya
Duniani, Geneva, Dk. Ivan Ivanov amesema kuwa Tanzania ina wafanyakazi zaidi
ya milioni 16 , wengi wao wakiwa kwenye sekta isiyo rasmi ambao ndiyo nguvu
kazi ya Taifa na chanzo cha kipato kwa jamii na Taifa.
Amesema
utafiti uliofanywa na mtaalamu aliyeteuliwa na WHO umebainisha changamoto
mbalimbali ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ili kuboresha maslahi na
mazingira ya kufanyia kazi kwa kundi hilo.
“Ninajua
wafanyakazi nchini Tanzania wamekuwa chanzo cha mapato, uzalishaji na ni
tegemeo kwa jamii na Taifa, wanapougua au kupata ajali kwa sababu ya mazingira
yasiyo salama hasara kwao wenyewe na kwa Taifa kwa kuwa hali hii inaongeza
idadi ya wafanyakazi wagonjwa” Amesema Dk. Ivanon.
Amesema
WHO inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuweka msisitizo katika
kuboresha mazingira ya wafanyakazi katika sekta zote ili kudhibiti mazingira
yenye viashiria hatarishi kwa afya za wafanyakazi maeneo ya viwanda, Sekta ya
Afya, migodini na mashambani.
Amesema
kuwa mchango wa WHO ikishirikiana na Tanzania ni kuboresha Mpango mkakati kwa
ajiri utakaowezesha uboreshaji wa Afya za wafanyakazi kuanzia ngazi ya ngazi ya
kijiji hadi Taifa ili kuwalinda wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye mazingira
hatarishi kwenye sekta isiyo rasmi wakiwemo watoto na wazee.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya na Usafi wa Mazingira wa wizara hiyo
Dk. Halid Masa akiuelezea mkutano huo wa wadau wa Afya na Usalama wa kazi
amesema kuwa unakusanya wadau wote nchini ili kupitia taarifa ya utafiti
uliofanywa na mtaalam aliyeteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema
kufanyika kwa utafiti huo kunatokana na Azimio la mkutano wa Afya wa dunia
(World Health Assembly) lililotoka mwaka 2007 ambao ulizitaka nchi zote
zitengeneze mpango wa utekelezaji kuhusu masuala ya Afya kazini.
Amesema
kupitia Azimio hilo Tanzania ilianza kufanya utafiti mwaka 2005 na ripoti ya
utafiti huo imekamilika tayari kwa majadiliano yanayowahusisha wadau ili waweze
kutoka na mkakati wa utekelezaji wa kukabiliana na changamoto za afya kazini.
“Mwaka
2005 utafiti huu ulianza kufanyika sasa umekamilika, kwenye mkutano huo
wameitwa wadau ili kupata taarifa hii, kuijadili na kutoka na mkakati wa pamoja
wa kukabiliana na changamoto zote za masuala ya Afya Kazini” Amesema.
Amesisitiza
kuwa suala la Afya kazini ni mtambuka kwa kuwa linahusisha wadau mbalimbali
pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo ufanyaji wa kazi katika mazingira
yasiyo salama.
Click here to Reply, Reply to all, or Forward 16.1 GB (107%) of 15 GB used Manage Terms - Privacy Last account activity: 0 minutes ago
0 Comments