Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiongea na wakazi wa Magomeni Kota kuhusu kumalizika kwa mgogoro wa makazi leo Jijini Dar es Salaam .Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula na Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo , Yamungu Kayandabila
Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
MAELEZO Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemaliza mgogoro wa makazi wa Magomeni Kota uliodumu kwa kipindi kirefu. Hayo yamesbainishwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati akiongea na Kamati ya Mgogoro wa Makazi ya Magomeni Kota mbele ya waandishi wa habari. “Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefuta hati na mikataba yote inayohusiana na ardhi ya yaliyokuwa makazi ya Magomeni Kota, Dar es Salaam”,alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi Rais ameondoa umiliki wa eneo hilo toka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kumilikisha Serikali Kuu ambayo ndiyo itakayosimamia ujenzi wa nyumba 644 ambazo zitauzwa kwa bei nafuu kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota.
“Tutajenga nyumba 644 na kuwauzia kwa bei ya jengo na siyo ya ardhi ili kuwapeni unafuu katika kununua,”alisema Lukuvi huku akishangiliwa na baadhi ya wakazi wa Magomeni.
Aidha, Lukuvi amesema kuwa anampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kumaliza mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa ameagiza timu ya wataalamu wa Wizara kupima na kuchora michoro kwa ajili ya ujenzi. Lukuvi amesema katika eneo hilo zitajengwa nyumba za heshima ambazo kila moja itakuwa na vyumba vitatu ili kukidhi mahitaji ya kifamilia kwani watu hawa wamekaa kwa miaka takribani 50 hadi wameshapata wajukuu.
Ameongeza kuwa kila mmiliki wa nyumba hiyo atapewa hati yake hata kama nyumba hiyo itakuwa kwenye ghorofa. Lukuvi amesema kuwa Rais ameagiza maeneo kama ya Magomeni Kota katika mikoa ishirini ya Tanzania Bara nayo yatakuwa katika mfumo huo wa Magomeni.
Kwa mujibu wa Lukuvi wazee ambao wanakaa kwenye nyumba kama hizo sehemu nyingine wasiondolewe kwani hao walikuwa watumishi wa umma hivyo Rais amesema wasibughudhiwe. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mgogoro wa Makazi Magomeni Kota, George Abel ameshukur Mhe Rais Magufuli na Wazir Lukuvi kwa kutatua mgogoro huo ambao anadai umewasumbua sana.
Ameahidi kutoa ushirikiana kwa Serikali pindi suala la ujenzi litakapokuwa linaendelea ili kuhakikishaujenzi unaenda haraka. Naye Wakili ambaye alikuwa akiendesha kesi hiyo kabla ya Mhe. Rais kuingilia kati, Mhe. Twaha Tasilima ameonyesha kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli.
“Rais Dkt Magufuli na Mhe. Waziri Lukuvi ni watu wa vitendo na si maneno na kweli wanawajali wanyonge, nawashukuru sana,”alisema Tasilima. Uamuzi wa kurudisha eneo hilo kwenye Serikali Kuu umetolewa na Rais Magufuli tarehe 10/7/ 2016.
0 Comments