NITAHAMIA DODOMA SEPTEMBA MWAKA HUU - WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  alipokuwa akiwasalimia na kuwashukuru mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma mapema leo asubuhi  waliojitokeza kushuhudia  maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.PICHA NA MICHUZI JR-DODOMA
*Asema akishahamia, Mawaziri na Naibu Mawaziri wote wafuatie mara moja
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba, mwaka huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Julai 25, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.
“Jana nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma ifikapo Septemba,” amesema na kushangiliwa na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo.
Amesema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kazi nyingi zimefanyika na wananchi wameziona na kwamba sasa hivi kazi iliyobakia ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
“Wananchi kazi mmeziona na sasa tunaenda kwenye utekelezaji. Ninatoa agizo kuwa mawaziri na manaibu wote wahame mara moja kutoka Dar es Salaam na kuja Dodoma. Wana ofisi ndogo Dodoma na kwa kuwa wamekuwa wakiishi wakati wote wa Bunge, wahamie mara moja. Mimi nahamia Septemba, na utekelezaji wake nitausimamia kwa juhudi zote,” alisisitiza.
Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kutunza amani ya nchi na kudumisha umoja uliopo na pia akataka watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na hoteli za kitalii ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.
Wakati huo huo, mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika muda wa siku tatu amerudia kusisitiza nia ya Serikali kuhamia  Dodoma katika kipindi chake cha uongozi ili kutekeleza ndoto ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka makao makuu ya nchi yawe Dodoma.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma kwenye uwanja wa mashujaa huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema atahakikisha Dodoma inakuwa makao makuu ndani ya miaka minne na miezi minne iliyobakia kwenye awamu ya kwnza ya uongozi wake.
“Kama wabunge karibu 300 na mawaziri na manaibu wao ambao hawafiki 30 wanakaa hapa kwa miezi mitatu na maisha yanakwenda, kama makao makuu ya chama kinachotawala nchi yako hapa sioni sababu ni kwa nini Serikali ninayoiongoza iendelee kubakia Dar es Salaam,” amesema.
Mara kwanza kutoa kauli hiyo, ilikuwa ni Jumamosi iliyopita, Julai 23, 2016 wakati akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkutano Mkuu maalum wa chama hicho.
Rais Magufuli amesisitiza wananchi na wanasiasa kutunza amani na kudumisha amani iliyokuwepo nchini. Pia amewataka Watanzania wote kuendelea kuwaenzi mashujaa walioipigania nchi hii.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,    
DODOMA.
JUMATATU, JULAI 25, 2016.

Post a Comment

0 Comments