27/07/2016
PRESS
RELEASE
KUFUNGIWA KWA MSANII NAY WA MITEGO KUJIHUSISHA
NA KAZI ZA SANAA KWA MUDA USIOJULIKANA
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana Msanii wa
muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego
hadi hapo litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na
Baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo
dhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Maagizo
aliyopewa Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha Shilingi milioni
1, kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata
sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya Sanaa kwa maana ya
kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.
Aidha,
Msanii Nay ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye
kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususan wanawake.
Maamuzi
haya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984,
ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari,
Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Adhabu
hizi zimetolewa kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu jana
siku ya Jumanne tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye kukiri makosa
na kuahidi kubadilika.
Makosa
aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;
1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo
kusajiliwa na BASATA.
2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia
katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.
3. Maudhui
ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni
kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.
Ikumbukwe
kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia
wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yenye uvunjifu mkubwa wa
maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha,
tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako wa
Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya. Hivyo adhabu hii imetolewa ili
kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama kweli ana nia ya
kuendelea kufanya kazi ya muziki
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
0 Comments