Nikianza na neno la shukrani, naomba nizitoe za dhati kwa kunivumilia, na kufanya nami kampeni ya Imetosha katika mazingira magumu sana katika awamu ya kwanza. Hii ni kutokana na ugeni katika uendeshwaji wa taasisi pamoja na uhalisia wa safari za kiharakati, mara nyingi wanaofika safari huwa ni wachache, lakini nyie hamkuwahi kukata tamaa katika kuniunga mkono.
Awamu ya kwanza ya
kutambulisha taasisi na misimamo yake imefanikiwa, na sasa tunaenda katika
awamu ya pili, ambapo baada ya kufanya matembezi, na kampeni mbali mbali
ndogondogo, tulifanikiwa kwa kuungwa mkono na taasisi rafiki na azma ya kwanza
ilikuwa ni kukiunga mkono kituo cha Buhangija kilichopo Shinyanga.
Lakini baada ya mimi
binafsi kama muasisi na mwenye wazo, kufikiri kwa kina kuhusiana na Shinyanga,
ambako kiukweli mazingira yake hayajathibitika kuwa salama, na pili kuwa ni
kituo cha serikali, nilikuja na wazo la Taasisi kuwa na kijiji cha mfano
ambacho, pamoja na kuhifadhi watu wenye ualbino na wasio na ualbino bali pia
kiwe kituo cha uzalishaji mali, ambacho kitawakomboa watu wenye ualbino katika
ile dhana na kuomba omba, na kuwa wachangiaji rasmi wa pato la taifa kwa
kufanya biashara ya kilimo na ufugaji.
Hivi ninavyoongea
tayari tumeshatoa malipo ya awali kwa Mzee idd Shemdoe wa huko Bumbuli,
Lushoto, mkoani Tanga ambaye amekubali kuiuzia taasisi shamba la Mikahawa lenye
ukubwa wa ekari 50. Hapo taasisi ina mpango wa kufungua kituo kitakachoitwa
Santa Lucia, Safe House and Estate.
Eneo litatumika kwa
kilimo, ufugaji, pamoja na elimu, kwa maana ya shule kubwa inayofundisha kwa
mtaala wa kimataifa, lengo likiwa ni kuwawekea watu wenye ualbino vitega uchumi
ambacho vitasababisha wao na taasisi yao kutowapigia wafadhili magoti mara kwa
mara na badala yake kuwa sehemu ya watatuzi wa matatizo ya kijamii
yanayoiklumba nchi.
Kaka na dada zangu,
kuwa na eneo tu haitoshi, na safari ya kuifikia ndoto hii ni ndefu inayochukua
muda mrefu kuikamilisha. Mimi naiamini kwa sababu tu nina nia na nimedhamiria
kuifanya kama sehemu ya ndoto zangu za kimaisha.
Nachukua nafasi hii
kuwaomba kunisaidia kushiriki katika shughuli mbali mbali nitakazokuwa
nazifanya katika kutunisha mfuko wa taasisi, na hapa naileta kwenu shughuli ya
Music and laughetrs, ambayo Orijino Komedi wamekubali kuwa wenyeji huku muziki
nao ukichukua sehemu kubwa ya shughuli.
Hii itakuwa Septemba
11, naomba muwahimize wadau kadri muwezavyo wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono
kwa umoja wetu.
Mungu
ibariki tanzania Mungu aubariki umoja wetu.
0 Comments