AADHA YA MBWENI JKT, KINONDONI

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

UPIGE mbizi. Ndivyo unavyoweza kusema msemo huu kama unahitaji kupita haraka haraka katika eneo la Mbweni JKT, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, mahala panapojengwa daraja la kuvukia watu kwa miaka mitatu sasa, halina dalili za kukamilika hivi karibuni.
 Ni eneo tata. Ni eneo linalokera na kusumbua watu mno. Mbaya zaidi, ni eneo lililozunguukwa na majumba ya watu wenye ukwasi au ukubwa wa majina ya viongozi waliojenga katika eneo hilo. Eneo linalojengwa daraja hilo ni kwenye mkondo wa maji unaotokea baharini.
Gari likivuka eneo la mkondo wa bahari, ambapo pia ndipo panapojengwa daraja hilo hatua chache mkono wa kulia kutoka gari linapopita. Maji yakijaa hapo hakuna kupita wala kuvuka.

Kwa wanaofahamu tabia za mikondo hii ya baharini watakuwa wanaelewa. Na wasiofahamu ni kwamba, linakuwa na tabia za kujaa maji na kupungua kila wakati. Kwa mfano, mtu anaweza kupita saa tatu asubuhi akakuka hakuna maji mengi. 

Lakini dakika kadhaa mbele, maji mengi yanajaa kutokea baharini. Ukifanya makosa, ukiwa na haraka ya kuendelea na shughuli zako, ndipo hapo unapopaswa upige mbizi.
Hapa ndipo panapojengwa daraja hili.

Uyavulie nguo, upite. Na ikiwa na una gari, huna budi kusubiri kwanza yapunguwe kama si kuisha kabisa maji hayo. Au utafute njia nyingine za kukufikisha eneo unaloelekea, ingawa njia hiyo ina usumbufu mkubwa wa muda na gharama nyingine pia. Ni kutokana na hilo, serikali kwa kupitia Halmashauri ya Wilaya Kinondoni, inapaswa kupigia jicho kuu eneo hili. Iangalie tatizo ni nini?

 Mbona daraja hilo halikamiliki kwa miaka mingi sasa. Hakuna kinachoendelea. Watu wanapata tabu. 

Mbaya zaidi ni eneo linalovutia na kusisimua, maana haiwezekani mtu ajenge nyumba mamilioni ya shilingi wakati njia ya kumfikisha kwake haieleweki eleweki. Ni wazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni pamoja na DC Paul Makonda wanapaswa kuliangalia suala hili kwa kina.

Kama serikali haina fedha za kukamilisha mradi huo iwachangishe wananchi wake, maana hii adha wanayokutanaa nayo ya kupiga mbizi si nzuri. 

Inapoteza muda. Inadhalilisha pia. Ikiwa mtu anasafiri nje ya nchi, anawahi uwanja wa ndege, anaweza kushindwa kusafiri kwa kuchelewa ndege yake kama atafika kwenye eneo hilo na kukuta maji yamejaa. 

Ni aibu na fedheha kubwa. Mtaa umezunguukwa na majumba ya mamilioni ya shilingi. Mtaa umezaja watu wengi wenye nazo, viongozi wakubwa, lakini njia wanayopita inapitika kwa vipindi vya maji kujaa na kuisha. Hii haiwezekani. 

Serikali iliangalie hili la mradi wa daraja la Mtaa Mbweni JKT, ambalo nalo pia linajengwa chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Post a Comment

0 Comments