Meneja
Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi
na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro akiwaeleza waandishi wa habari
(hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu kueneza Mkakati wa
Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa kwa Wanafunzi wa Manispaa ya
Kinondoni na Temeke baada ya kumaliza Manispaa ya Ilala. Kulia ni Afisa
Habari wa Idara ya Habari Maelezo Bi Fatma Salum.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakisikiliza taarifa ya mafanikio kutoka kwa
Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro leo jijini Dar es Salaam.
Picha na MAELEZO.
**********************
Na Fatma Salum- Maelezo
Jumla
ya wanafunzi 15,120 wa shule za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya
Ilala jijini Dar es Salaam wameweza kusajiliwa na kupata vyeti vya
kuzaliwa kupitia Mkakati wa Usajili na Kutoa Vyeti vya Kuzaliwa
unaotekelezwa na Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hayo
yamesemwa na Meneja Masoko, Mawasiliano na Elimu kwa Umma kutoka
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Josephat Kimaro wakati
wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
“Mkakati
huu umeonesha mafanikio makubwa kwani mpaka sasa wanafunzi 15,120
wamepata vyeti vya kuzaliwa wakiwemo wasichana 7,712 na wavulana 7,408
kutoka shule 201 za Manispaa ya Ilala ambapo 201 ni shule za Msingi na
96 ni Sekondari.” Alisema Kimaro.
Akifafanua
zaidi kuhusu mkakati huo uliozinduliwa mwezi Aprili mwaka huu Kimaro
alisema umelenga kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwapatia
wanafunzi vyeti vya kuzaliwa wakiwa shuleni badala ya wazazi kuvifuata
kwenye Ofisi za RITA.
Aidha
umesaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu
umuhimu wa cheti cha kuzaliwa kwani wazazi wengi wameshawishika kufanya
usajili na kupata vyeti kwa ajili ya familia nzima.
Pia
Kimaro aliongeza kuwa baada ya mkakati huo kufanikiwa katika Manispaa
ya Ilala RITA inatarajia kuendeleza katika Manispaa za Temeke na
Kinondoni mnamo mwezi Januari 2015 zikifuatiwa na Manispaa nyingine za
Tanzania Bara.
Akitoa
wito kwa wazazi na walezi Kimaro amewataka kutumia fursa hiyo kuwapatia
vyeti watoto wao wanaosoma katika shule ambazo program inatekelezwa
kwani hutumia mfumo rahisi kwa gharama nafuu na mtoto hupata cheti
halisi.
0 Comments