Wakati
vikao vya Bunge Maalum la Katiba vikiendelea tena mjini Dodoma wiki hii
bila ya kuwepo kwa kikundi kinachojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samweli Sitta amesema amekuwa
akisisitiza kuwa bunge hilo halitaahirisha shughuli zake hadi hapo muda
wa siku 60 waliopewa utakapokamilika.
Sitta
alisema rasimu hiyo ina mambo mengi mazuri lakini pia akasema kuna mambo
mengine yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili Watanzania waweze kupata
katiba bora.
Ni
kweli kwamba maudhui ya rasimu ya katiba yanajumuisha baadhi ya mambo
yafuatayo; kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora wa mamlaka ya
Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano, kuimarisha haki za
binadamu na kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa.
Naamini
upo ukweli kwamba ndani ya rasimu hiyo inayojadiliwa yapo mapungufu kwa
kuachwa masuala ya kuwezeshwa kuundwa kwa Serikali za Mitaa, maelekezo
ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine.
Hakika
kitendo kinachofanywa na wajumbe wa bunge hilo wanaounda Ukawa ni
kibaya kwani kususia kikao si jambo jema na badala yake wangelumbana kwa
hoja ndani ya bunge.
Niwaombe
tu wana Ukawa kwamba waache kupotosha umma na kuonekana kuwa wao ni
bora zaidi ya wajumbe wengine walioko ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kanuni, Pandu Amir Kificho tayari amewasilisha mapendekezo
ya kanuni 12 ambazo zitaliwezesha bunge hilo kukamilisha kazi yake
katika muda uliopangwa wa siku 60.
Mapendekezo
hayo yalipitishwa katika moja ya kikao cha jioni wiki iliyopita kwa
kauli moja kutoka kwa wajumbe waliokuwepo na hivyo kazi ya kuanza
kujadili sura zilizobaki zikaanza na zitaendelea wiki hii.
Kwa
kumbukumbu zangu ni kwamba awali akichangia mapendekezo hayo, mjumbe wa
bunge hilo na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala alisema kuundwe
kanuni itakayowabana wajumbe waliotoka katika Bunge hilo na hata wajumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph
Sinde Warioba iliyoshughulikia mchakato wa ukusanyaji maoni kutoingilia
mwenendo wa bunge hilo wakati huu vikao vyake vinapoendelea.
Ni
jukumu la wapenda amani wote katika nchi hii kuwahimiza Ukawa kuingia
katika meza ya maridhiano kwa sababu muda bado upo na ni vizuri sana
wakaingia sasa bungeni kwa sababu yanayojadiliwa yanawagusa wananchi
katika majimbo yao moja kwa moja.
Nizidi
kumuomba Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe kuliona hili na kukumbuka
wahenga waliosema kuwa hakuna vita inayokwisha nje ya meza ya
mazungumzo. Hii ni hoja yangu, muitafakari tafadhali. Wanachi wote
wanataka Katiba mpya itakayodumu miaka 50 ijayo.
0 Comments