JK afungua ukumbi wa mihadhara CHUO cha SEKOMU, aagiza wilaya zote nchini zijenge maabara katika kila shule



 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete Mkuu wa Chuo cha Sebastian Kolowa Memorial University SEKOMU  Askofu Dr.Stephen Munga(kushoto)Makamu Mkuu wa Chuo cha SEKOMU Dr.Anneth Munga(watatu kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa(kulia) wakikata utepe kuzindua rasmi ukumbi wa mihadhara wa Benjamin William Mkapa wilayani Lushoto 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kuwasili katika Chuo Kikuu chA Sebastian Kolowa Memorial University mabapo alifungua ukumbi wa mihadhara na kuhutubia wananchi.Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha SEKOMU Askofu Dr.Stephen Munga na kulia ni makamu wa chuo Dr.Anneth Munga.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwasililiza kwa makini wanafunzi kutoka Irente school for the Blind wakati walipoimba shairi maalumu wakati wa sherehe za ufunguzi wa ukumbi wa mihadhara wa Benjamin William Mkapa katika  chuo kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial University SEKOMU
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wanafunzi wa wageni waliohudhuria sherehe ya ufunguzi wa ukumbi wa mihadhara wa Benjamin William Mkapa uliofanyika katika chuo kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial University SEKOMU huko Lushoto Mkoani Tanga

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Wananchi kuhakikisha kuwa ifikapo Mwezi Novemba Mwaka huu,  kila Shule ya Sekondari katika maeneo yao, ina  maabara kwa ajili ya masomo ya Sayansi.

Rais Kikwete amesema hayo Mkoani Tanga katika nyakati tofauti Wilayani Kilindi na Lushoto ambapo yuko katika ziara ya kikazi Mkoani Tanga tangu tarehe 8 Julai hadi tarehe 12 Julai,2014.

"Nataka ifikapo Mwezi Novemba, Mwaka huu vyumba vya maabara viwe vimekamilika, tulipeana miaka miwili, imetimia" Rais amesema na kuongeza kuwa lazima tusahihishe makosa tuliyofanywa ya
kutojenga maabara wakati tunajenga shule za sekondari nchini kote.

Mwaka 2006, Serikali ilihamasisha ujenzi wa Shule za Sekondari nchini kote na muitikio ni mzuri, lakini hakukuwa na uhamasishaji wa kujenga maabara. “Tumeamua kushughulikia suala la maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi kote nchini." Rais amesisitiza.

Rais amesema ameridhika na upanuzi wa Elimu katika ngazi za Msingi na Sekondari kote nchini na Serikali inaendelea na hatua ya kutatua changamoto za ubora wa Elimu, kuongeza Walimu, kuongeza Vitabu, ujenzi wa Maabara na Nyumba za Walimu kote nchini.

 Akihutubia katika mkutano wa hadhara Wilayani Lushoto Rais ameahidi kuboresha na kushughulikia suala la ujenzi wa barabara ya kwenda Bumbuli na zaidi kuhakikisha anaweka barabara ya lami katika mji wa Lushoto na mji mdogo wa Bumbuli.

Rais anaendelea na ziara Wilayani Lushoto na Mkinga ambapo anaendelea kuzindua miradi na kukagua miradi ya maendeleo.

Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
10 Julai,2014

Post a Comment

0 Comments