BALOZI IDDI AKAGUA MRADI WA VISIMA KIJIJI CHA UZI NA NG'AMBWA


 Baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na Ng'ambwa  wadogo kwa wakubwa wakiendelea na harakati za matengenezo ya Bara bara yao itokayo Unguja Ukuu hadi Uzi kila baada ya kupuyngua kwa kina cha maji.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja     Ukuu – Uzi Bwana Shaya Mohd akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif eneo lenye kupitisha maji mwengi ambayo huleta kadhia kwenye Bara bara yao.
Katibu wa Kikindi cha Ushirika cha Hapa Kazi chenye wanachama 48 katika Kijiji cha Uzi ambae ni Mlemavu Bibi Mwanajuma Harufu Haji akimnon’oneza Kitu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kuzungumza na wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa 
 Moja ya Visima vichache vilivyomo ndani ya Kijiji cha N’gambwa ambavyo vina upungufu mkubwa wa maji kiasi kinachochangia kuleta usumbufu wa huduma hiyo ndani ya Kijiji hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika Picha ya Pamoja na wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Uzi mara baada ya kuzungumza na wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa. Kulia ya Balozi mwenye kilemba ni Mbunge wa Jimbo la Koani Mh. Amina Andrew na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Nd. Ramadhan Abdulla Ali. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
********************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuifanyia utafiti wa kina  na hatimae kusaidia kugharamia ujenzi wa kudumu wa Bara bara  itokayo Unguja Ukuu kuelekea Uzi Kisiwani yenye urefu unaokadiriwa kufikia Kilomita Mbili Nukta Sita ambayo hivi sasa bado iko katika kiwango cha mawe matupu.
Ombi hilo limetolewa na Wananchi wa Vijiji vya Unzi na N’ambwa mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ndani ya Jimbo la Koani kuangalia maendeleo na matatizo yanayowakabili wananchi wa Jimbo hilo liliomo ndani ya Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif Ali Iddi akipata wasaa wa kuikagua kwa kina Bara bara hiyo ya Unguja Ukuu hadi uzi ambapo Wananachi wa Vijiji hivyo chini ya Mwenyekiti wao wa  Ujenzi wa Bara bara hiyo Mzee Shaya Mohd hawakuchelea kumuelezea kadhia  wanayopambana nayo wanapovuka sehemu hiyo hasa wakati wa maji Makuu.
Mzee Shaya Mohd alifahamisha kwamba Wananchi wa Vijiji hivyo wamefikia hatua ya kukata tamaa  kutokana na kadhia ya maji yanayosababisha  kupangua mfumo wa mawe licha ya juhudi kubwa wanazozichukuwa katika kupanga mawe hayo katika kila baada ya kipindi kifupi.
Alisema baadhi ya wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa hasa akina Mama wajawazito wakati mwengine hulazimika kujifungulia njiani kutokana na kadhia ya Bara bara hiyo jambo ambalo huleta hatari kwa mazingira ya mzazi na motto mwenyewe.
“ Bara bara yetu iliwahi kufanyiwa Utafiti na hatimaye kujazwa mchanga katika  katika Bara bara hii katika miaka ya thamanini lakini kilichojitokeza mara baada ya  kupunguwa kwa kiwango cha maji makuu mchanga wote uliowekwa umekwenda na maji hayo “. Alifafanua Mzee Shaya Mohd  Haji.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi            Uzi - N’gambwa alifafanua kwamba njia pekee ya kukabiliana na tatizo hilo kulingana na mfumo wa maji ya bahari yanayokata katika eneo hilo ni kutumiwa kwa saruji,kokoto na mawe kwenye ujenzi wa Bara bara hiyo ili iweze  kudumu kwa kipindi kirefu katika matumizi yake.
Akielezea kadhia ya ukosefu wa huduma  ya Maji safi na Salama ndani ya  Kijiji cha N’gambwa naye Mzee wa Kijiji hicho Bwana Khatib Mussa alimsikitikia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Wananchi wa Kiji hicho wanashindwa kuendelea vyema na harakati zao za kimaisha kutokana na muda mwingi kuutumia katika kutafuta huduma hiyo.
Mzee Khatib Mussa alifahamisha kwamba huduma za maji safi ambazo ziliwahi kufika Kijijini hapo katika miaka michache iliyopita lakini hivi sasa zimekatika kabisa na kuifanya jamii ya kijiji hicho kuwa katika mazingira ya hatari  kiafya.
Akizungumza na Wananachi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa  kwa nyakati tofauti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Miundo Mbinu Zanzibar kuiweka katika Bajeti yake ya Mwaka Ujao Bara bara hiyo ili Serikali  ipate fursa ya kuitengea fedha za ujenzi.
Balozi Seif  aliwahakikishia Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona  matatizo yanayowakabili wananchi wake katika maeneo mbali mbali hapa Nchini yanapatiwa ufumbuzi wa kina.
“  Kwa kweli tunataka kuona  Vijiji vya Uzi na N’gambwa ndani ya Jimbo la Koani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja vinabadilika  na kuwa vya kisasa ili vilingane na vijiji vyengine hapa Nchini “. Alieleza Balozi Seif.
Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliahidi kuchangia Matofali 1,000 pamoja na saruji Mifuko 10 kwa ajili ya kuongeza nguvu za ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Uzi linalotayarishwa kwa ajili ya wanafunzi watakaoingia Elimu ya Sekondari hapo mwakani.
Balozi Seif pia akaahidi kuzipatia seti moja moja na mipira miwili kwa kila Timu za Soka za Wanawake wa Vijiji vya Bungi na Kidimni pamoja na kuitaka Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu Uzi kufanya makisio ya ujenzi wa Banda la Hifadhi wakati wa kujaa kwa maji liliopo kwenye jiwe kubwa la Kihistoria kati kati ya Bara bara hiyo.
Naye Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdullah Shaaban akitoa ufafanuzi katika Mkutano wa Hadhara wa Wananachi hao juu ya tatizo la Maji safi na Salama  Uzi na N’gambwa alisema  Wizara hiyo iko katika hatua za mwisho kutafuta Pampu kubwa itakayokuwa suluhu ya tatizo hilo.
Hata hivyo Waziri Shaaban alifahamisha kwamba katika juhudi za kuisaidia nguvu Pampu hiyo wataalamu wa Wizara hiyo wanatarajia pia kujenga Tangi la Maji kati kati ya Vijiji vya Uzi na N’gambwa ambalo litakuja kusaidia kusambaza kwa uhakika huduma hiyo.
Akisoma Risala ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Vijiji hivyo Ndugu Abdu Mohd Khamis alisema  Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi Uzi tayari umeshagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia 166,019,000/- hadi sasa.
Ndugu Abu Mohd alisema kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 124,633,000 ni nguvu za Wananchi, Shilingi Milioni 25,786,000 zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Koani na Shilingi Milioni 15,600,000 zikatolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo la Koani.
Alisema wananchi wa Vijiji hivyo wameishukuru Idara ya Ujenzi wa Bara bara Zanzibar { UUB } kwa hatuzake za mashirkiano na wananachi hao yaliyopelekea kwa kiasi kikubwa kuwawezesha kuitumia kwa unafuu Bara bara hiyo.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Maendeleo alisema Vijiji hivyo pia vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa huduma za Umeme ambalo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif tayari ameshaiagiza Wizara inayohusika na masuala ya Umeme kulibeba jukumu hilo kwa kutafuta nguzo 10 na waya zake ili kuliondosha tatizo hilo.

Post a Comment

0 Comments