WANACHAMA YANGA KUAMUA HATMA YA KLABU YAO, KUWA KAMPUNI AU KUBAKI KLABU




UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanzisha mchakato wa kupiga kura kwa wanachama wake kuamua hatma ya klabu yao kuwa kampuni au kubaki kama klabu ya soka ya kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu wa klabu hiyo, Lawrance Mwalusako ilisema kuwa wanachama hai wote watakuwa na haki ya kupiga kura na kutoa maamuzi yao.
Mwalusako alisema kuwa maamuzi hayo ni utekelezaji tu wa kile walichoamua katika mkutano wa Wanachama uliofanyika 16 Januari, 2013 ambapo Mwenyekiti kwa niaba ya Kamati ya Utendaji aliwapa Wanachama wafikirie mapendekezo ya Yanga kuwa Kampuni ama kutokuwa Kampuni kisha kuyawasilisha kwa katibu mkuu wa Yanga.
Katibu huyo alisema kuwa anaamini kuwa wanachama wamefikiria vya kutosha hivyo kuanzia leo 16 Oktoba, 2013 mpaka 10 Novemba, 2013, kutakuwa na sanduku moja (1) klabuni kwa ajili ya kukusanya kura za maoni ambapo wanachama wanaotaka Yanga kuwa kampuni watapiga kura ya (NDIYO) au wasiopenda wataandika (HAPANA)
Alisema kila mwanachama hai atakuwa na uhuru wa kupiga kura na atalazimika kuja na Kadi yake ambapo itamzuia kupiga kura mara mbili au zaidi. Zoezi hili ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya YANGA.

Post a Comment

0 Comments