Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WADAU wa mambo ya utamaduni na michezo wameombwa kujitokeza
kwa wingi kufanikisha kufanyika kwa Tamasha la Utamaduni lililopangwa kufanyika
Desemba 14 mwaka huu wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Mratibu wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga, Kambi Mbwana, pichani.
Hayo yamesemwa na mratibu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana,
alipozungumza na mwandishi wa mtandao huu mapema leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache
baada ya kutangaza mipango ya kuandaa tamasha hilo la aina yake na lenye mguso
wa kuwakutanisha wadau wote kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo, Mbwana alisema
endapo wadau wote, wakiwamo wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni, taasisi za
serikali watashirikiana katika hilo, mambo yatakuwa mazuri.
Alisema hali hiyo inamfanya aone haja ya kuwataka watu hao
washirikiane kwa pamoja kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tamasha la utamaduni na
michezo Handeni linafanyika kwa mafanikio na kuweka historia mpya.
“Watu wote wana umuhimu katika kufanikisha kwa tamasha hili,
hivyo kila mmoja kwa nafasi yake tunaomba msaada wake hata wa kimawazo,
ukizingatia kuwa kinachofanyika kwa sasa ni kuachiana majukumu tu.
“Tunawaomba wote wenye moyo wa kufanikisha wazo hili
tushirikiane nao kwa namna moja ama nyingine, hasa kwa kuona wenye kampuni zao,
mashirika na taasisi za serikali pia kutudhamini katika hili,” alisema Mbwana.
Kwa mujibu wa Mbwana, kufanyika kwa tamasha hilo kutakuwa ni
sehemu nzuri ya kuwakutanisha wadau, wananchi wa Handeni na Tanzania kwa ujumla
kwa ajili ya kujadiliana changamoto zinazowakabili kwa maendeleo yao.
Tamasha hilo la Utamaduni linaandaliwa chini ya Raha Company
and Entertainment huku likifanyika kwa mara ya kwanza katika wilaya hiyo
inayoongozwa na Mkuu wake wa Wilaya Muhingo Rweyemamu, wakati mbunge ni Dk
Abdallah Omari Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
0 Comments