MKURABITA YAPANIA KULETA MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA KWA VITENDO.



 By. Pascal Mayalla           
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania, MKURABITA,  unaendelea na  utekelezaji kwa vitendo, wa awamu ya kwanza ya kuwapatia  “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania” kwa kuendelea  kugawa
hati miliki za kimila  kwa wanavijini mbali mbali, ili kwanza kuwamilikisha rasilimali, kasha ndipo kuwaelimisha jinsi ya kuzitumia rasilimali hizo kujiletea maendeleo ambayo ndiyo yatakayo leta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa  Mkurabita, Bibi. Seraphia Mgembe, wakati akitoa tathmini ya zoezi la kuwakabidhi hati miliki za kimila, kwa wakulima wa zao la chai wa wilaya ya Mbinga, Mufindi na Njombe, lililohotimishwa hivi karibuni.
Bibi Mgembe amesema, maisha bora kwa kila Mtanzania, haya patikana kwa wananchi kubweteka na kuisubiria serikali ndio ifanye kila kitu, bali ni kwa serikali kujenga mazingira ya uzalishaji mali, ikiwemo kuwamilikisha wananchi rasilimali zao, na maendeleo ya kweli, yatapatikana kwa wananchi kuelimishwa na kujibiidisha katika kutumia
rasilimali hizo kama dhamana za kupatia mitaji ya kujiletea maendeleo.
Bibi Mgembe amesema,  huku zoezi la kuwamilikisha wananchi rasilimali zao likiendelea, MKURABITA inayapitia tena yale maeneo ambayo tayari wananchi wake wameisha kabidhiwa hati miliki, ili kuwajengea uwezo wananchi hao, jinsi ya kuzitumia hati miliki hizo kama dhamana na kukopa katika mabenki ili kutumia  fedha za mkopo kujiletea maendeleo.
Bibi Mgembe amesisitiza, maendeleo ya kweli na endelevu, ni yale yanayotokana na  matumizi ya rasilimali zilizowazungunguka wananchi husika,  nan i kwa kulitambua hilo, ndio maana MKURABITA imekuwa ikizishirikisha taasisi za kifedha, ili kuwaelimisha wananchi fursa mbalimbali za mikopo ya kibiashara na kimaendeleo zinazoweza
kupatikana kwa kutumia dhamana za hati miliki zao.
Kwa upande wao, Wakuu wa wilaya za  Njombe, Bi. Sarah Dumba na Mkuu wa Mufindi, Bi. Evarista Kalalu, waliipongeza MKURABITA kwa juhudi zake za kuhakikisha wakulima wa chai sasa wanayamiliki rasmi mashamba yao ya chai, ambapo  mwanzo walikuwa na utajiri ambao hauwafaidii chochote zaidi ya kulima na kuuza mazao yao, lakini sasa, sio tuu ni wamiliki wa mashamba hayo, bali wanaweza kuzitumia hati miliki zao, kukopo mikopo mikubwa ya kimaendeleo.
Jumla ya hati miliki za kimila zaidi ya 2000 zilikabidhiwa kwa wakulima wa chai.
 Wananchi wa Njombe, wakifurahia kukabidhiwa hati miliki za kimila, kulikofanywa na MKURABITA hivi karibuni.
 Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, akimkabidhi hati miliki ya kimila, Mwanakijiji wa kijiji cha Matembwe, Bw. Solomon Matunasa wakati wa hafla fupi ya MKURABITA kukabidhi hati miliki za kimila kwa wakulima wa chai wa Rungwe, Mfindi na Njombe hivi karibuni. Katikati ni Mratibu wa MKURABITA, Bibi Seraphia Mgembe.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, akimkabidhi hati miliki ya kimila, Mwanakijiji wa kijiji cha Iwafi, Bw. Eneas Paruasi wakati wa hafla fupi ya MKURABITA kukabidhi hati miliki za kimila kwa wakulima wa chai wa Rungwe, Mfindi na Njombe hivi karibuni. Katikati ni Mratibu wa MKURABITA, Bibi Seraphia Mgembe.

Post a Comment

0 Comments