Rais wa IBF katika bara la
Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi amewasili
katika jiji la Gaborone, Botswana kupromoti ubingwa wa IBF wa Kimataifa katika
uzito wa Bantam.
Bondia wa Botswana Lesley Sekotswe na bondia mwenzake kutoka
nchini Namibia Immanuel “Prince” Naidjala walitoka sare wakati wakishindania
ubingwa huo katika pambano lililofanyika katika jiji la Windhoek, Namibia
tarehe 20 Mei mwaka huu.
Ujio wa Rais Ngowi ulikuwa unangojewa na wadau wengi wa
ngumi katika nchi hii tangu aitembelee Botswana mwaka 2002 wakati wa mpambano
kati ya bondia wa Botswana Thuso Kubamang na Peter Malinga kutoka nchini Afrika
ya Kusini.
Rais Ngowi atakutana na viongozi wa serikali ya Botswana
pamoja na wadau mbalimbali wa ngumi na safari yake itaanzia jiji kuu la
Gaborone mpaka jiji la pili kwa ukubwa la Francistown ambako wadau wengi wa
ngumi wanamsubiri kwa hamu.
Nchi ya Botswana ni nchi yenye msingi mzuri sana wa ngumi za
ridhaa lakini tatizo kubwa limekuwa ni namna ya kuwaendelza wanapofikia kikomo
kwenye ridhaa. Kikao cha Ngowi na viongozi wa serikali wa Botswana kitaweka
msingi mzuri wa namna ya kuwaendeleza mabondia wa Botswana.
Botswana ni nchi inayopakana na Namibia kwa hiyo mpambano wa
Sekotswe na Naidjala unategemewa kuwa na wapenzi wengi wa ngumi kutoka katika
nchi hizi mbili.
0 Comments