Watanzania wametakiwa kuweka tofauti zao mbali na
kuishangilia timu ya Simba inapocheza mechi yake ya marudiano na Libolo ya
Angola Jumapili hii kuwania kufuzu katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Wito huo umetolewa na wadhamini wa Timu ya Simba,
Kilimanjaro Premium Lager, kupitia Meneja Masoko Fimbo Butallah wakati wa kutoa
vifaa kwa timu ya Simba tayari kwa mechi hiyo kama sehemu ya udhamini.
“Wanapokwenda kwenye mechi hii hawandi tu kama Simba bali
wanaenda kuiwakilisha Tanzania kwa hivy0 ni muhimu kwa watanzania wote kuungana
na Kilimanjaro Premium Lager kuleta hamasa ili timu yetu iibuke na ushindi na
kusogea mbele katika mashindano haya,” alisema.
Alisema wao kama wadhamini wana imani kuwa Simba imejiandaa
vizuri na watafanya maajabu na kuibuka na ushindi ugenini.
“Mechi hii ni ngumu lakini tuna imani watafanya vizuri na
kuwafurahisha watanzania,” alisema Bw Butallah.
Akipokea vifaa hivyo Msemaji wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga
aliishukuru Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini wake mnono ambao umekuwa na
manufaa makubwa kwa klabu yao.
“Zawadi ambayo tunaweza kuwapa wadhamini wetu ni kushinda
Jumapili,” alisema Kamwaga.
Alisema watanzania wasiwe na wasiwasi kwani Simba ina uwezo
wa kufanya ilichofanya kwa Zamalek miaka kumi iliyopia kwani Zamalek ilishinda
Tanzania lakini katika mechi ya marudiano Simba ikashinda.
“Kuna wakati pia Zambia ilitufunga mabao manne nyumbani lakini
tulivyoenda kwa tukawafunga matano,” alisema Kamwaga.
Simba inatarajiwa kuondoka Ijumaa alfajiri kuelekea Angola
tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili.
Kilimanjaro Premium Lager ni mdhamini wa timu za Simba na
Yanga na Timu ya Taifa (Taifa Stars).
0 Comments