KESI YA 'LULU' YAAHIRISHWA HADI JULAI 9 2012

UMRI wa Msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael ‘Lulu’ unaendelea kupigwa danadana baada ya leo asubuhi upande wa Jamhuri katika kesi hiyo kukimbilia Mahakama ya Rufani kuomba uhalali wa Jaji wa Mahakama Kuu kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Kwa sababu hiyo Jaji Dk. Fauz Twaib alishindwa kuendelea kusikiliza kesi hiyo ambayo pande zote zilishapeleka ushahidi wake hivyo ilikua kazi ya jaji huyo kufanya uchunguzi na kutoa uamuzi wake.
Katika mdai yake kwa Mahakama ya Rufani upande wa Jamhuri umeeleza kwamba kitendo anachotaka kufanya jaji Dk. Twaib si halali na kwamba kulikua na upungufu wa kisheria hivyo kuitaka mahakama hiyo kusema iwapo ni halali ama la.
Akiahirisha kesi hiyo hadi Julai 9 mwaka huu jaji huyo alizitaka pande zote zisubiri iwapo faili la kesi hiyo litaitwa Mahakama ya Rufani huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama ukihoji sababu za Jamhuri kukimbilia Mahakama ya Rufani jana huku ukieleza kwamba kulikua na muda wa kutosha kufanya hivyo.  
Awali Mwanasheria wa Serikali Elizabeth Kaganda aliomba apewe muda wa dakika 10 ili aangalie iwapo faili la kesi hiyo limeitwa Mahakama ya Rufani akidai kuwa yapo masuala yanayohitaji mwongozo wa mahakama hiyo.
Nje ya mahakama hiyo wakili mwingine wa utetezi katika kesi hiyo Peter Kibatala alidai kwamba wakati kesi ilipokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu waliomba mshitakiwa apewe haki sawa na mtoto ombi lililopingwa na upande wa Jamhuri kwa maelezo kwamba mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza ombi hilo. 
“Sisi tumewasilisha uthibitisho kuhusu umri wa Lulu na upande wa Jamhuri nao tulisikia wamefanya hivyo leo tukaja kwa ajili ya uamuzi lakini imekuwa ndivyo sivyo,” alilalama wakili Kibatala.
Lulu anatuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba yaliyotokea Aprili 7, 2012 huku upande wa utetezi ukidai kwamba msanii huyo ana umri wa chini ya miaka 18 jambo linaloendelea kuzua ubishani mahakamani.
Katika kesi hiyo upande wa jamhuri unaongozwa na Kaganda akishirikiana na Shadrack Kimaro wakati Fungamtama, Kibatala na Fugency Massawe wakimtetea Lulu.

Post a Comment

0 Comments