FAUDHIA ABDILLAH
Na Kaka Mwinnyi
MSANII chipukizi katika anga ya filamu nchini, Faudhia Abdillah a.k.a Sifa, amewataka waigizaji wakongwe wa fani hiyo kukaa chonjo baada ya kukamilisha kazi yake ya 'muvi' mpya inayokwenda kwa jina la ‘Chini ya Jua’ ambayo itaingia sokoni mwezi ujao.
Sifa ametema cheche hizo mwishoni mwa wiki iliyopita , amesisitiza kuwa watakaoiona filamu hiyo watakiri uwezo wake baada ya kwenda sambamba na nyota kama Flora Mvungi, Badra, Katambo Kiki, Basupa, Bega na wengine kuigiza filamu hiyo.
"Ninamaanisha, sisemi kwa kujifagilia wala kubahatisha nimefanya kazi nzuri ambayo inafaa kuwapa changamoto waigizaji wazoefu katika fani naamini nimeigiza katika kiwango cha juu ukizingatia ndiyo kazi yangu ya kwanza kwani hata akina Flora Mvungi na Badra walinikubali na kunitia moyo kwa kunitabiria kuwa nitakuwa mkali zaidi hapo baadaye," alisema Sifa.
Filamu hiyo iliyotengezwa na Kampuni ya Farasi Entertainment ya jijini Dar, imetungwa na Rashid Ngayana maarufu kama Pete ambaye pia ni Muongozaji na Mtayarishaji muziki na kuchukuliwa picha zake katika miji ya Tanga na Dar es Salaam.
Pete, alisema kuwa filamu yake imebeba ujumbe mzito kwa jamii kuhusu usaliti wa mapenzi ambapo mwanamume anaamua kulipa kisasi kwa wahusika waliomtorosha mpenzi wake hadi Ulaya kwa kuwaua. Anamuua daktari aliyemtoa mimba, dereva taksi aliyempeleka uwanja wa ndege na mpambe (Badra) aliyemshawishi kutoroka na mikasa mingi mingine.
0 Comments