TIMU YA TAIFA U20 (Kilimanjaro Boys)
KOCHA Mkuu wa timu za Taifa za vijana, Kim Poulsen leo ametangaza kikosi cha
wachezaji 30 wanaounda timu yenye umri chini ya miaka 20 (Kilimanjaro Boys) kwa
ajili ya michuano mbalimbali ya kimataifa.
Poulsen ambaye kwenye Kilimanjaro Boys anasaidiwa na Adolf Rishard amesema timu
hiyo pia itashiriki michuano ya Kombe la Uhai itakayofanyika Novemba mwaka huu.
Michuano ya Uhai inashirikisha U20 za timu za Ligi Kuu ya Vodacom.
Amesema Kilimanjaro Boys itakuwa ni ya kuingia na kutoka kwa wachezaji kwani
kigezo kikubwa cha kuchezea timu ni kiwango cha mchezaji, hivyo anatarajia
yatakuwepo mabadiliko ya mara kwa mara.
Kocha huyo amesema lengo ni kuwa na wachezaji 50, hivyo ataendelea kuteua
wengine kupitia michuano ya Rollingstone inayofanyika Arusha na vilevile
wachezaji watakaosajiliwa katika timu za pili (U20) za klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom ambazo usajili wao unafikia tamati kesho (Julai 20 mwaka huu).
Poulsen amesema timu hiyo kama ilivyo U17 itakuwa inafanya mazoezi ya wiki moja
kila mwezi, kuanzia Agosti ambapo pia itakuwa inacheza mechi moja ya kirafiki.
Amesema angependa U17 nayo ishiriki michuano ya Kombe la Uhai, lakini uamuzi juu
ya hilo unabaki kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Pia amesema
U17ambayo ilishachaguliwa kupitia michuano ya Copa Coca Cola inatarajia
kushiriki mashindano ya CECAFA yanayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu
Nairobi, Kenya.
Poulsen amesema mahali popote ambapo kutakuwa na mchezaji anayefaa kwa timu hizo
anaomba afahamishwe ili aweze kumfuatilia kabla ya kuamua kumchukua au la.
Wachezaji walioitwa Kilimanjaro Boys ni makipa Juma Ally Seif (Kombaini ya
Ilala), Saleh Malande (TSA) na Jackson William Wandwi (Azam). Mabeki ni Hassan
Khamis Kessy (Mtibwa Sugar), Khamis Mroki (Mtibwa Sugar), Yassin Omary (Polisi
Dodoma), Andrew Kassembe Mathew (Simba), Issa Rashid Issa (Mtibwa Sugar), Ally
Feruzi Teru (Simba), Said Ruhana Samir (Kagera Sugar), Samuel Mkomola (Azam),
Eric Mawala (Moro United) na Amani Kyata (TSA).
Viungo ni Madenge Ramadhan (JKT Ruvu), Frank Damayo (JKT Ruvu), George
Mtemahanji (Italia), Seme Omega Sunday (Yanga), Ibrahim Rajab Juma (Azam),
Abdallah Kilala Hussein (AFC Arusha) na Rajab Zahir (African Lyon).
Washambuliaji ni Ayoub Saleh Kitala (Ruvu Shooting), Atupele Green Jackson
(Yanga), Thomas Ulimwengu (AFC Sweden), Michael Victor Mgimwa (Mtibwa Sugar),
Jerome Lambele (Moro United), Simon Msuya (Simba), Ramadhan Suzana Singa
(Simba), Alex Joseph Setty (Majimaji), Renatus Leopold Patrick (Polisi Dodoma)
na Edward Christopher (Simba).
Boniface Wambura
Ofisa Habari.
0 Comments