BALOZI TEMBELE ASHIRIKI MDAHALO MAALUM KUADHIMISHA MIAKA 70 YA MKUTANO WA ASIA NA AFRIKA

Balozi wa Tanzania nchini Indonesia   Mhe. Macocha  Tembele leo tarehe 16 ,Aprili, 2025 ameshiriki katika mdahalo maalum wa maadhimisho ya miaka 70 ya Mkutano wa Asia na Afrika  maarufu kama Mkutano wa Bandung. 

Mdahalo huo umeandaliwa na Kituo cha Mikakati na Masomo ya Kimataifa (Center for Strategic and International Studies- CSIS) cha Indonesia ambapo mdahalo  huo  umehudhuriwa na Mhe. Arif Havas Oegroseno, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na  wanafunzi . 

Kwa upande wake Mhe. Balozi Tembele pamoja na mambo mengine amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo  zilizoshiriki kikamilifu katika utekelezaji wa misingi ya ushirikiano , mshikamano, usawa na ukombozi zilizoasisiwa katika nkutano wa Bandung wa mwaka 1955 kupitia ushiriki wake katika uanzishwaji wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM), pamoja na harakati za ukombozi wa nchi za Afrika. 

 Balozi Tembele amezungumzia kuhusu umuhimu wa mataifa ya ulimwengu wa kusini kudumisha fikra za Bandung kwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kupitia Taasisi na Jumuiya zake za Kikanda kama vile Umoja wa Afrika (AU) na ASEAN. 

 Wakati huohuo Mhe. Balozi ametoa wito kwa nchi za ulimwengu wa Kusini kuangalia uwezekano wa kuzifanyia mapitio agenda za Bandung ili ziweze kuakisi hali ya sasa ya kidunia na kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani kwa kujumuisha maeneo mapya ya ushirikiano kama vile mabadiliko ya tabianchi

Post a Comment

0 Comments