Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sayansi) Prof. Simon Msanjila Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es salaam.
Washiriki wa Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki kutoka nchi 9 za Bara la Afrika wakifuatilia Mkutano wa mtandao huo leo jijini Dar es salaam.
Washiriki wa Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki kutoka nchi 9 za Bara la Afrika wakifuatilia Mkutano wa mtandao huo leo jijini Dar es salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki .
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka akiwaeleza
waandishi wa Habari kuhusu mpango wa Serikali wa kupima na kurasimisha maeneo
yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam leo.
Na. Aron Msigwa – Dar es
salaam.
Serikali imewataka wataalam
wa vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Usimamizi wa Ardhi waitumie taaluma yao
katika kutafuta suluhisho la migogoro ya Ardhi inayowakumba wananchi katika
maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kwa Niaba
ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wakati wa Ufunguzi
wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo
jijini Dar es salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sayansi) Prof. Simon
Msanjila amesema kuwa wataalam hao wanalo jukumu la kufuatilia migogoro
inayotokea nchini na kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalam utakaotoa majibu ya
utatuzi wa migogoro hiyo.
“Ninyi kama watalaam wa
sekta ya Ardhi lazima mtoe majibu kwa nini migogoro ya ardhi inaendelea kutokea
katika maeneo mbalimbali licha kuwepo kwa kanuni, Sheria na taratibu
zinazosimamia sekta ya Ardhi nchini” Amesema Prof.Msanjila.
Ameeleza kuwa wao kama
watalaam wa sekta hiyo wanatakiwa kwenda zaidi kwenye matatizo halisi na kuwawafikia
wananchi wengi zaidi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuondoa changamoto zao kuliko kucheza na
vitabu na kuongea kwenye Ofisi.
Amewataka wataalam hao hasa wale walioko
nchini Tanzania kufika katika maeneo yenye migogoro ya Ardhi ikiwemo Morogoro
na maeneo mengine ili kuangalia kwa nini wananchi wanaendelea na mapigano tunajua
ipo migogoro ya Ardhi inayotokea katika mikoa ya Morogoro, Pwani na mikoa
mingine.
Amesema kuwa kwa upande
wa Serikali suala la ufumbuzi wa migogoro ya Ardhi linaendelea kupewa
kipaumbele kwa kuhakikisha kuwa ardhi inaendelea kutolewa kwa kuzingatia sheria
pia kushughulikia changamoto zote zinazokwamisha ustawi wa sekta ya ardhi
hususan uondoaji kero zote zinazokwamisha matumizi bora ya ardhi kwa jamii.
Akifafanua kuhusu
nafasi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi katika
mkutano huo ameeleza kwamba kupitia mkutano huo wa kitaalam wa masuala ya Ardhi,
Wizara hiyo inajifunza kuhusu changamoto
zitakazojitokeza na kuibuliwa ili ziwekwe kwenye mitaala kwa lengo la kuwaandaa
watalaam watakaokuwa na uwezo wa kusuluhisha matatizo yote yanayojitokeza
kwenye sekta hiyo.
Amesema kuwa Sekta ya
Elimu kupitia mkutano huo itaboreshwa kwa kupata nyongeza ya utalaam kutoka kwa
wataalam kutoka Vyuo vikuu vya nchi mbalimbali za Bara la Afrika waliohudhuria
mkutano huo na kuongeza kuwa Chuo Kikuu Ardhi nchini Tanzania ambacho kimebobea
kwenye masuala ya Ardhi kitapata taarifa zaidi katika uboreshaji wa mitaala na
mafunzo ya Programu za Utawala wa Ardhi, Ugawaji wa Ardhi na Upimaji wa Ardhi”
Kwa Upande wake Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza mara baada katika
mkutano huo amesema kuwa wataalam wa Ardhi nchini Tanzania bado wana umuhimu
mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Ardhi na kufafanua kuwa wao kama chuo
kinachozalisha watalaam wa Ardhi wanalo jukumu kuzalisha watalaam watakaofanya
usimamizi thabiti wa Ardhi kukabiliana na changamoto zilizopo.
“Sisi nafasi yetu kama
Chuo Kikuu Ardhi ni kujua ni namna gani tunavyoweza kuzalisha wataalam wa
kutosha wenye weledi watakaoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizoko
kwenye sekta ya Ardhi pia kuhakikisha wataalam tunaozalisha wanakidhi ubora na
matarajio ya wananchi” Amesema Prof. Mshoro.
Amesema kuwa
wanataaluma kutoka Tanzania watanufaika kutokana na mkutano huo kwa kuwa unawajumuisha
watalaam wa Ardhi kutoka takribani nchi 9 watakaobadilishana uzoefu kuhusu
changamoto mbalimbali za ardhi zinazojitokeza katika maeneo yao na namna
wanavyozitatua.
Aidha, amesema kuwa
Sekta ya Ardhi nchini Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa watalaam wa
kutosha ambao wangeweza kusimamia
maamuzi katika masuala ya Ardhi ngazi za chini na kuongeza kuwa ili kupata
maamuzi na taarifa sahihi za ardhi ni lazima suala la uwepo wa watalaam hao
liendelee kupewa kipaumbele.
Kuhusu mchango wa
watalaam hao katika utatuzi wa migogoro ya Ardhi amesema kuwa ipo haja ya
watalaam waliopo kutumika ipasavyo kutatua migogoro inayojitokeza na kuwaletea
manufaa wananchi ambao wanahitaji huduma za wataalam hao.
Amesema kuwa kwa
upande wa Serikali tayari watalaam wa sekta husika wamejipanga kuhakikisha kuwa
wanapata suluhisho la mgogoro inayojitokeza kupitia sheria zilizopo.
Mkutano huo unaohusisha Mtandao wa vyuo Vikuu ni wa nane tangu kuanzishwa Mtandao wa EALAN mwaka 2009 ambapo kwa mwaka huu Chuo Kikuu Ardhi, Tanzania kimekuwa mwenyeji wa Mkutano huo kufuatia kuteuliwa kuwa kituo Maalum Cha Mafunzo ya Usimamizi wa Ardhi Barani Afrika.
0 Comments