Benki ya Biashara ya Akiba (Akiba Commercial Bank) imeahidi
kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanamichezo wa Mtandao wa Wasanii Tanzania
(SHIWATA) waliojenga nyumba katika kijiji chao cha Mwanzega, Mkuranga.
Akizungumza kwenye mkutano wa wanachama wa SHIWATA
wanaomiliki nyumba 185 zilizojengwa katika kijiji cha wasanii na wengine
waliogaiwa mashamba ya kilimo, Meneja wa Benki ya ACB tawi la Ilala, Mary Haule
aliwahakikishia kuwapatia mikopo ya ujenzi, na ufugaji kwa muda mfupi.
Alisema mikopo hiyo itawawezesha wanachama hao kujenga
mabwawa ya kufuga samaki, kufuga kuku na
kuboresha nyumba zao kuwa za kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib akimtambulisha Meneja
Masoko wa Kampuni ya kuuza vifaa vya umeme wa jua, kutoka Kampuni ya Steps,
Maulid Said wanachama hao walihakikishiwa kuingiza umeme wa jua kwa gharama ya sh. 250,000 kila nyumba.
Msanii Faridu Taratibu aliwaambia wenzake kuwa safari ya
kuhamia kijijini alikuwa ameianzisha na
sasa anahamia baada ya huduma zote za awali za jamii kama umeme zitafikishwa
kijijini.
SHIWATA katika mkutano huo ilitoa nafasi nyingine kwa
wawekezaji kujenga shule, zahanati, na maduka mbalimbali ya vifaa vya ujenzi na
vyakula.
Mtandao huo unaomiliki eneo la ekari 300 za makazi na ekari
500 za kilimo imepata baraka za Serikali ya wilaya ya Mkuranga katika jitihada
za kuwakomboa wasanii wake.
Mwenyekiti Taalib alisema SHIWATA imeweka mikakati kwa
wanachama wake watakaohamia kijijini kupewa ekari moja bure ya kulima mazao
yatakayowawezesha kupata mbogamboga na mazao ya muda mfupi.
0 Comments