Na. Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mbunge wa Ubungo (CHADEMA) Saeed Kubenea kifungo cha nje cha miezi mitatu kutokana kosa la kutumia lugha ya matusi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo leo Jijini Dar es Salaam Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Thomas Simba amesema kuwa mahakama imeamua kumpa mshitakiwa adhabu ya kifungo hicho kwa kuwa ndilo kosa lake la kwanza, hivyo Mshatakiwa anastahili kupata adhabu ya huruma. Chini ya adhabu hiyo iliyotolewa chini ya kifungu no 89 kifungo kidogo cha kwanza Mhe.
Kubenea hatakiwi kufanya kosa la aina yoyote ambalo litamsababisha arudishwe tena mahakamani na endapo itatokea akafanya hivyo mahakama itampa adhabu ya kifungo cha kwenda jela.
Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo mshtakiwa Said Kubenea mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba alipewa nafasi ya kujitetea ni kwanini asipewe adhabu kali kwa kosa alilolitenda ambapo alieleza Mahakama hiyo kuwa hakuwa na nia mbaya ya kwenda kufanya fujo eneo la tukio ambapo kulikuwa na mgomo wa wafanyakazi wa kiwanda cha nguo cha TOOKU cha jijini Dar es salaam bali alikwenda kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgomo huo akiwa kama mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Ubungo.
Ikumbukwe kuwa Jalada la kesi hiyo na 320 ya mwaka lilifunguliwa na Jamhuri dhidi ya Said Kubenea kwa kosa la kutumia lugha ya matusi kwa aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda, Aidha upande wa washtakiwa wameonyesha kutoridhishwa na hukumu hiyo na wameomba kukata rufaa.
0 Comments