WALIMU ILALA WATANGAZA MGOMO


NA KHADIJA KALILI,DAR ES SALAAM
CHAMA cha Walimu Mkoa wa Ilala  (CWT –Ilala) jijini  Dar es Salaam kimepanga kufanya maandamano makubwa na ya kihistoria ikiwa ni katika  kudai haki yao ya msingi ya malimbikizo ya fedha za walimu wastaafu na likizo.
Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Ilala, Emmanuel Kihako alitoa msimamo huo jana Oisini kwake , akimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ajitayarishe kuyapokea maandamano hayo ya walimu wote wa kutoka katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo Ilala.
Aidha, Kihako amewataka walimu wote wajiandae kisaikolojia  kufanikisha maandamano hayo huku akisema kwamba hawataondoka kwenye ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala hadi atakapowapatia majibu ya kueleweka na yenye  utekelezaji na siyo maelekezo kama jinsi ilivyokuwa huko nyuma.
“Kimsingi ni kwamba, tunaunga mkono hoja ya Rais wa CWT, Gracian Mukoba aliyoitoa mapema mwezi uliopita jijini Dar es Salaam, ambapo aliitaka serikali itoe uamuzi kuhusu malimbikizo ya fedha za walimu kabla ya uchaguzi mkuu, hivyo na mimi ninasema kwamba maandamano yetu yatafanyika kabla ya uchaguzi ikiwa ni kwa ajili ya lengo la kuishinikiza serikali itulipe madai yetu,” alisema Kihako.
Kihako anaongeza kwa kusema kwamba walimu wa Tanzania wanasikitishwa na serikali kwa kuwapuuza wakati wao ndiyo nguvu ya umma, hivyo imekuwa ikiwafanyia vitendo vya ukatili kama kulimbikiza madeni ya walimu huku wabunge wakilipwa fedha nyingi na kwa wakati tofauti na ilivyo kwa walimu.
Alisema hiyo ni kutokana na walimu kutolipwa nauli zao za likizo na wengine 76 ambao ni wastaafu hawajalipwa  mafao yao ya kustaafu kama walivyostahili, hivyo wastaafu hao wamekuwa wakinung’unikia serikali, huku akisema fedha ambazo wanaidai serikali ni kiasi cha shilingi bilioni 1  na milioni 368,331.
Katika suala la likizo, alisema changamoto kubwa ni kutolipwa likizo zao kati ya Juni na Desemba 2014, jambo linalochangia manung’uniko miongoni mwa walimu hivyo kushusha ari ya kufanya kazi na kufundisha katika ubora unaotakiwa, hivyo kuchangia hata kiwango cha elimu nchini kushuka.
Pia aliongeza kwa kusema kuwa walimu wanapokuwa na manung’uniko hushusha ari ya utendaji kazi  pia kuichukia serikali yao.
Kihako alisema kwamba siku yeyote kuanzia leo watakutana na Kamati  ya Uendeshaji ya Wilaya ya Ilala, ili kushauriana kufanya mambo ya msingi kwa chama na walimu ili kutoa ushawishi wa kufanya maandamano makubwa hadi kwa  mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
“Mimi ndiye nitakayeongoza maandamano hayo  na hatutatoka hadi madai yetu ya msingi  yatakapotekelezwa kwa vitendo, hivyo nawaomba walimu wote wa shule za msingi na sekondari zilizoko Ilala wajiandae ili tudai haki  zao, kwani tumekuwa wavumilivu  sana katika kudai haki zetu,” alisema Kihako.
Aliongeza kwa kusema kuwa anawaomba wawakilishi wote wa Ilala nao wajiandae kisaikolojia pia amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi kama ataona kuna sababu yeyote ya kuwasaidia anaweza kuwasaidia kwani lengo kubwa ni kuhakikisha haki ya mwalimu inapatikana.

Post a Comment

0 Comments