Na
Ally Daud
MAELEZO, Dar
Es Salaam.
07.09.2015
IDADI ya mauzo katika
soko la hisa la Dar es salaam (DSE) imeshuka
kwa asilimia 78 kutoka Tsh. Bilioni 29.8 hadi Tsh. Bilioni 6.4 kwa
kipindi cha wiki moja iliyopita.
Aidha idadi ya hisa
zilizouzwa katika soko hilo pia zimeshuka
kwa asilimia 60 kutoka Tsh. Milioni11.2 hadi kufikia Tsh. Milioni 4.3 kutokana na
makampuni mengi kutowekeza katika soko la hisa.
Akizungumza na
waaandishi wa habari leo (Jumatatu Septemba 07, 2015) Meneja Miradi na Biashara
wa DSE, Patrick Mususa alisema kuwa hata hivyo idadi ya mtaji katika soko umekuwa
kutoka tilioni 21.8 hadi tilioni 21.9 ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya mtaji
wa makampuni ya ndani kutoka Tsh. Trilioni
9.7 hadi Tsh. Trilioni 9.9.
Aidha Bw.Mususa
ameitaja benki ya CRDB kuwa ndiyo inayoongoza kuuza hisa zake katika soko hilo ikiwa
na asilimia 91, ikifuatiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ikiwa na asilimia 7
na Benki ya NMB ikiwa na asilimia 0.5.
Kwa mujibu wa Mususa
alisema kampuni ambazo zinaongoza kwa ongezeko la bei katika soko la hisa kuwa ni
Uchumi Super Market ikiwa na asilimia 5.5 ikifuatiwa na Benki ya KCB ikiwa na asilimia
4.4 pamoja na benki ya NMB 3.5
“Viashiria vya soko katika
huduma za kibenki vimeongezeka kwa alama 62, hisa za benki ya NMB zimeongezeka kwa pointi 3.5 ikifuatiwa na sekta
ya viwanda kwa alama 20 kutokana na ongezeko
la bei ya hisa za TBL”
Mususa alifafanua kuwa pamoja
na viashiria vya kibiashara kushuka kwa alama 4 kulikochangiwa na punguzo la
bei ya hisa za swissport kwa asilimia 0.13, kwa ujumla kiashilia cha soko kimeongezeka.
“DSE tumeboresha huduma
zetu kwa kuanzisha huduma ya kimtandao ya DSE mobile Trading ili kuwawezesha watumiaji wa huduma hizo kujiunga
, kununua na kuuza hisa kupitia simu ya mkononi kwa kupiga *150*36#”.
0 Comments