Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Hamis Kigwangalla akitangaza nia yake ya kugombea urais waJamhuri ya Muungano ya Tanzania wakati alipokutana na waandishi wa habari kwenye ambapo amesema hajasukumwa na mtu yeyote ila ni yeye mwenyewe ameamua kwa moyo wake. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Hamis Kigwangalla akimtambulisha mke wake Dr. Bayoum Awadh wakati wa mkutano huo.
Baba Mzazi wa Dr. Kigwangalla Nassor Kigwangalla na mama yake mzazi
Mchungaji Patrick Saso akifanya maombi kabla ya kuanza kwa mkutano huo. |
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
............................................................................................
............................................................................................
Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni heshima kubwa sana kwangu
kupata fursa hii. Ni katika nchi chache sana duniani, mtoto wa maskini
kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani akiuza karanga, Big G, maandazi,
jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata chochote kwa ajili ya
kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi yake. Kwamba, mtoto
aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari. Hii inamaanisha misingi
ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili haikuwa
ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi. Kwamba,
siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe kipaji chako.
Hili peke yake linanipa sababu ya
ziada ya kwa nini nitamani kuota kuwa Rais – nataka niwe mfano hai wa
mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali nani
anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni
lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania
itakayodumu kwenye misingi hii: kwamba sisi sote ni ndugu, na tuna fursa
sawa. Kwamba, kuendelea kimaisha na kibinafsi ni haki ya binadamu na si
hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie kama nilivyokuwa mimi hapa, ana
haki na fursa ya kuwa mbunge ama Rais wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa
Mbunge.
Kwa namna ya kipekee nichukue
fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa kusimamia
tunu hizi. Niwashukuru pia viongozi wote walionitangulia kwa kuzilinda,
na niahidi nitakuwa wa mwisho kuisaliti nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo nimefika hapa kwa sababu chama
change kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na
Wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa
sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama
changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Leo nazungumza hapa
nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itatoa uongozi wa Taifa letu katika
awamu ijayo.
Babu yangu Kizaa Baba aliishi
Kijijini Goweko, Mlimani, na alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina
asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya heshima sana pale
kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi
kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye CCM
katika ngazi ya Kata.
Babu yangu na Bibi yangu kizaa
mama waliishi Nzega, na ndiyo walionilea baada ya ndoa ya mama yangu na
baba yangu kuvunjika. Walinifundisha mambo mengi, kubwa likiwa ni
kujiamini, pia kufanya mambo yangu kwa bidii, uadilifu, umakini na kwa
nidhamu ya hali ya juu. Bibi yangu huyu hakusoma shule ya kizungu
japokuwa alijifunza kusoma na kuandika. Babu yangu alikuwa mjukuu wa
Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora School miaka miwili mbele
ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini
ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za kuanzishwa na
kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”,
na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe
dhidi ya wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na
hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama yangu aliishia
kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania
ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa
ajili ya mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki, naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya
maisha yangu ni mfano hai kwa maisha ya watanzania wengi. Na kwamba,
nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda
ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia. Naliona jukumu la
kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la
kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Kazi yangu imenifikisha sehemu
nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na
watu wa kila aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata
mmoja kati ya watu hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake
zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na
wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa
kule Pugu Road viwandani, kwa watumishi pale hospitali ya Taifa
Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo kwa wafanyabiashara, wote
watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na wachache pale TRA,
ama kulipa posho za bure kwa wabunge na mawaziri kule Bungeni, kulipia
mashangingi ya viongozi na watendaji, kulipia tiketi za ndege daraja la
kwanza kwa ajili ya safari za viongozi na wataalamu wetu kwenda
kujifunza kupambana na umaskini wakati wakirudi wanauacha uzoefu uwanja
wa ndege, ama kulipia semina, warsha na makongamano ya wataalamu ya
kuandika sera za MKUKUTA, MKURABITA na kuandaa bajeti zisizotekelezwa
kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda kule kwa watani zangu,
Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa ndugu zangu kule Nduli, Kyela, wazee
kule watakuambia hawategemei Serikali itawaletea ubwabwa kwenye sahani
za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua
kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo
siku zote. Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki
shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza
uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi,
waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu,
wanahitaji, mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na
bila kudhulumiwa wala kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali itabeba
mizigo yao yote. Lakini wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu
vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali, tukibadili
kidogo namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa,
kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na wajukuu zetu.
Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu kutoka miongoni mwa nchi maskini
kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu
wengi, nina imani kubwa kabisa, kwamba tunaweza kubadili mustakabali wa
Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha bora zaidi kwa
watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi kwa matumaini,
kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia leo. Tutaweza
kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na
kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi
kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya
mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu,
tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya ninayoyasema si
ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa
tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya
haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi
sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye,
tutafanikiwa.
Nyote mliopo hapa na
wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa ukaribu
sana, kututathmini na kutupima sote; tuliojitokeza hadharani, walioanza
safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa
ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi watanzania, kuwa kati
yetu sote, ni nani anafaa kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza
kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari
wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara
kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua
aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini
katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa
na Katiba, anayeamini katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari
kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini
katika Haki ya kupata huduma bora za afya, elimu, maji, kama
wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata mahakimu na
majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza
kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki hizi bila kutazama hali
zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini
zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili
kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba
na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya
watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya
uchumi, masoko na biashara za hasara na faida za makampuni makubwa ya
kimataifa nje ya mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili
tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila
athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu.
Kuwa, ni nani miongoni mwetu
anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio wengi, historia yake,
rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi
‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila
kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na
kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari wangu. Na ninayasema haya,
haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina: mahitaji ya sasa na
baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya kugombea na
kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari,
kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia
utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu, na zaidi nia yangu ya kuwa
sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika
nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya namna
tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia
utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama Taifa.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais
nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo
wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa mkono
si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na
wala si kwa daraja langu kwenye jamii, dini yangu, ama kabila langu.
Ninaamini nitapimwa kwa sifa na uwezo wangu, kama mtanzania.
Watanzania tuna sifa moja kubwa;
kwenye mambo ya msingi ya kitaifa, tunakubaliana kuwa maslahi ya
Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu binafsi. Tudumishe utanzania wetu.
Ninaamini katika Ndoto ya
Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Tanzania tuna kila sababu
ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia wameandaa
misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu cha
kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi
inayotokana na ndoto za wazee na waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko
tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi, maana naamini
tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu
wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana
na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira
kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa
mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na
umakini wa hali ya juu.
Mimi ninaamini kwamba, kama hata
mimi nimefika hapa, basi kila mtanzania anaweza, na ana haki ya kufika
hapa na kwenda mbele zaidi yangu. Mafanikio siyo haki ya wachache, ni
tunu ya Mwenyezimungu kwa kila mtu. Ninaamini ni haki ya kila mtanzania
kuota ndoto yake, kuifanyia kazi na kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ina wajibu wa kutoa fursa kwa watu wake kuota ndoto zao na
kufikia mafanikio bila kukwama.
Na ndugu watanzania wenzangu,
amini nawaambia, kuwa, mbele yetu tuna kazi ya ziada ya kufanya. Kazi
ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo tunao, sababu tunazo na nia
tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya
uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa
na raha kama wengine wanateseka. Ninaongozwa na ile dhana kwamba,
matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na si yangu peke yangu, ni yetu
sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho cha njaa ya
familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu
na familia yangu, hata kama siyo familia yangu.
- Kucheleweshewa haki ya
kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu
pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee Makame wa kule
Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na yeye hana nguvu
za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili asukume siku,
inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu yangu.
- Mama John ni mpishi
mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi mtaani kwake maeneo
ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo; akifukuzwa, akapigwa virungu,
akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na
mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya biashara mahala
pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama
yangu.
- Kama kuna mtoto
asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini kwa watani zangu warangi,
hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.
- Bwana Kalumanzila ni
mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo zake kumi kwa
kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza anachukua
kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa ya mwenye
mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata inamfanya
aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na
akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia
bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu.
Shida na madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa
sana moyoni, hata kama yeye si mjomba wangu.
Tarehe 4, Agosti 2014, Rais
Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha kimataifa cha maendeleo (Center for
Global Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa
mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini. Raslimali ya gesi inatoa
nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi
nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye
ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais
wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa
Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania
kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.
0 Comments