Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said (wa pili kulia) akipokea jezi mpya kutoka NMB
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
BENKI
ya NMB imeingia mkataba wa udhamini wa miaka miwili na mabingwa wa ligi
kuu soka Tanzania bara, Azam fc, utaohusisha gharama za usafiri na
baadhi ya nyingine za uendeshaji wa timu.
Mwenyekiti
wa Azam fc, Said Muhammad Said amewaambia waandishi wa habari leo makao
makuu ya klabu hiyo yaliyopo, Azam Complex, Mbande, Chamazi, nje ya
jiji la Dar es salaam kuwa mkataba huo utaanza utekelezaji mara moja.
“Tumeupokea kwa furaha mkataba huu na tunapenda kuwashukuru NMB kwa kuungana nasi”. Alisema Said.
Naye
katibu mkuu wa Azam fc, Nassor Iddrisa ‘Father’ alifafanua kuwa NMB
watanufaika na mkataba huo kwa kutangaza nembo yao katika jezi za Azam
fc, mabasi ya Azam fc na kuweka mabango katika uwanja wa Azam Complex.
Pia Azam watavaa jezi zenye nembo ya NMB kuanzia mazoezini na katika mechi za ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
Kwa
upande wake mkurugenzi mkuu wa NMB, Mark Weissing amesema mafanikio ya
Azam fc ndio chachu ya kuingia ushirikiano na timu hiyo.
Azam
fc inakuwa timu ya pili kuingia mkataba na taasisi ya kifedha nchini
ambapo timu ya kwanza ni Simba ambayo iliingia mkataba na NMB mwaka
2004, lakini 2004 walitemana.
Pia
NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kati ya
mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye
kwasasa ni kocha mkuu wa Yanga sc.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba baina ya Azam fc na NMB, watu wengi walikuwa na hamu ya kujua una thamani gani.
Hata
hivyo viongozi wa Azam fc waligoma kutaja thamani ya mkataba huo,
lakini taarifa za uhakika zinasema mkataba huo unakadiriwa kuwa na
thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.
Imeelezwa kuwa kwa kila mwaka Azam fc watanufaika na shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka NMB.
Tangu imeanzishwa mwaka 2004 ba kupanda ligi kuu 2008, Azam fc inapata mdhamini kwa mara ya kwanza .
Azam fc inakuwa miongoni mwa timu chache za Tanzania zinazonufaika na udhamini.
Simba
na Yanga ndio timu pekee zilizokuwa zinanufaika na udhamini, kwa miaka
mingi, lakini siku za karibuni Mbeya City walivuna milioni 360 kutoka
kwa Binslum.
Udhamini
ni moja ya vyanzo vya mapato kwa klabu za mpira wa miguu, lakini
imekuwa changamoto kwa timu mbalimbali kufikia mafanikio ya kupata
wadhamini.
Siku zote mdhamini anawekeza sehemu anayoweza kunufaika, hivyo sio rahisi kuweka fedha kwenye timu yenye kiwango kibovu.
Kilio
cha kukosa udhamini kwa timu za ligi kuu kinasikika kila kukicha,
lakini zimeshindwa kutegua mtego huo tofauti na Azam fc na Mbeya City.
Hakuna
haja ya kulia kwa kukosa udhamini, ukiucheza mpira kwa nafasi uliyopata
na kufanikiwa kama Mbeya City, Azam fc, Yanga, na Simba, mabilioni na
mamilioni yatakuja yenyewe.
Mafanikio
ya Azam fc yamewafanya walambe mabilioni kutoka NMB, na timu nyingine
zinatakiwa kujipanga kwa kutafuta mafanikio uwanjani zaidi ya kulia kila
wakati.
0 Comments