MSHAMBULIAJI wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameipeleka
timu yake katika fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil 2014 baada kufunga
mabao matatu ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sweden.
Mchezo huo ambao uliwakutanisha mastaa wawili ambao
ni manahodha wa timu hizo, Ronaldo anayeichezea Real Madrid na Zlatan
Ibrahimovic anayekipiga katika timu ya PSG ya Ufaransa wote walikuwa wanawania
nafasi ya kucheza fainali hizo pamoja na timu zao.
Ronaldo ambaye ndiye mfungaji wa bao la pekee katika
mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita nchini Ureno, alifunga bao la kwanza
dakika ya 50 kabla ya Ibrahimovic kusawazisha dakika ya 68.
Ibrahimovic aliongeza bao la pili dakika ya 72
lakini dakika tano baadaye Ronaldo alimaliza matumaini ya Sweden kucheza
fainali hizo mwakani baada ya kufua bao la pili.
Wakati Sweden wakisaka bao la kuongoza ili wafufue
matumaini ya kucheza fainali hizo, Ronaldo alizima kabisa ndoto hizo baada ya
kupachika bao la tatu dakika ya 79 na kufanya mchezo huo umalizike kwa jumla ya
mabao 4-2.
Nayo ufaransa imefanikiwa kutinga katika fainali hiyo
baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wake dhidi ya Ukraine shukrani
mabao ya Mamadou Sakho dakika ya 22, Karim Benzema dakika ya 34 na bao la
kujifunga na Oleg Gusev dakika ya 72.
Timu nyingine zilizofanikiwa kutinga katika fainali hizo ni Ugiriki ambayo ilitoka sare na Romania ya mabao 1-1 lakini imefuzu kwa jumla ya mabao 4-2, wakati Croatia nayo wamepenya katika hatua hiyo baada ya kuifumua Iceland mabao 2-0.
0 Comments