MASHAUZI KUTAMBULISHA MPYA IDD EL HAJ DAR WEST TABATA




Na Mwandishi Wetu
Bendi ya taarabu ya Mashauzi Classic kesho (Jumatano) itatambulisha nyimbo zao mpya kwenye onyesho maalum ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Hajj katika ukumbi wa Dar West Park, Tabata.
Onyesho hilo ambalo linajulikana kama ‘Usiku wa Isha Mashauzi’, imeandaliwa na Keen Arts na  Bob Entertainment chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi, Straika, Kwetu Mbambabay  na Saluti5.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga amesema kuwa onyesho litakuwa la kipekee na maalum kwa kusherehekea sikukuu ya Idd El Hajj.
Amesema katika onyesho hilo, Mashauzi atatambulisha albamu yake mpya ijulikanayo kama “Asiyekujua Hakuthamini” ambayo ina nyimbo kama “Mimi Bonge la Bwana,” utunzi wake Hashim Said, “Ropokeni Yanayoyahusu” ( Saida Ramadhani) na “Haya ni Mapenzi Tu” (Zubeda Malik).
Zawadi mbalimabli zitatolewa kwa mashabiki wa bendi hiyo inayojulikana kama Wakali wa Kujiachia.
“Tumeandaa zawadi mbalimbali kwa mashabiki wetu. Pia bendi ya Mashauzi Classic watatumia onyesho hilo kutambulisha nyimbo zao mpya,” Kapinga alisema.
“Mashauzi Classic watapiga albamu zao zote. Matumaini yetu ni kuwa watu watapata burudani ya kutosha kuliko siku zingine zote,” alisema Kapinga.
Nyimbo zingine zitakazopigwa ni  “Viwavijeshi” (Issa Ramadhani), “Sitasahau Yaliyonikuta” (Abdul Malik), “La Mungu Halima Mwamuzi” (Zubeda Malik) na “Sijamuona Kati Yenu” (Rukia Juma).
Naye mkurugenzi wa bendi hiyo, Isha Mashauzi, alisema kuwa onyesho la Da West litakuwa la kihistoria na kutaka watu wajitokeze kwa wingi ili historia isiwapite.
“Kwa kweli bendi iko fiti,” alisema Mashauzi.

Post a Comment

0 Comments