Na Mwandishi Wetu, Gaborone
TIMU ya soka ya vijana ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, inatarajia kurejea nyumbani kesho Ijumaa alfajiri ikitokea jijini hapa ambapo ilikuwa inashiriki kwenye mashindano ya vijana ya COSAFA ambayo leo yanaingia katika hatua ya nusu fainali.
Ngorongoro Heroes iliyokuwa kwenye kundi C ilimaliza hatua ya makundi ikiwa katika nafasi ya pili baada ya kutoka sare na Zambia na Afrika Kusini na ikishinda mchezo mmoja dhidi ya Mauritius uliofanyika juzi.
Zambia ambao ndio mabingwa watetezi wa mashindano haya ndio timu iliyofuzu kutoka kundi C huku yosso wa Afrika Kusini wakimaliza wakiwa kwenye nafasi ya tatu na Mauritius ikishika mkia.
Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Kim Poulsen, alisema jana kuwa ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mashindano haya na kusema kwamba wamejifunza mambo mengi ikiwemo uchezaji wa timu nyingine ambazo wanaweza kukutana nao kwenye mashindano mengine ya kimataifa.
Kim alisema kuwa mechi zote zilikuwa ngumu na wachezaji walijipanga kuhakikisha hawapotezi mchezo jambo ambalo limewasaidia kutofungwa.
Aliongeza kuwa kila mchezaji alionyesha uwezo wake na wale ambao ilikuwa ni mara ya kwanza kushiriki katika mashindano ya kimataifa wamepata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Issa Rashid, ambaye anachezea klabu ya Mtibwa Sugar inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, alisikitika kuona wametolewa kwenye mashindano hayo na kushaanga kutokuwepo kwa hatua ya robo fainali wakati ni mashindano yanayoandaliwa na shirikisho lenye uwezo.
Wakati huo huo, mechi za hatua ya nusu fainali ya mashindano ya vijana ya umri chini ya miaka 20 yanayoandaliwa na COSAFA inaanza leo jijini hapa kwa wenyeji Botswana kuikaribisha Zambia mchezo utakaofanyika kuanzia saa tisa mchana kwenye uwanja wa Molepolole ulioko nje kidogo ya jiji.
Botswana ilifuzu kutinga hatua hiyo juzi baada ya kuifunga Swaziland magoli 3-0 wakati Zambia yenyewe iliingia hatua hiyo kwa kuipa kichapo cha magoli 5-1 timu ya Afrika Kusini ambayo ndio timu pekee iliyokuwa inajiamini kwamba italibeba kombe hilo.
Nusu fainali nyingine itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Malawi dhidi ya Angola ambayo itaanza kurindima kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Mbali na Tanzania timu nyingine zilizotolewa ni pamoja na Swaziland, Afrika Kusini, Msumbiji, Namibia, Madagascar, Mauritius, Shelisheli, Lesotho na Zimbabwe.
Zambia ndio bingwa mtetezi wa mashindano hayo akiushikilia ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.
0 Comments