Social Icons

Tuesday, August 16, 2016

BASATA YAMFUNGULIA NAY WAMITEGO , WAMWEKA CHINI YA ULINZI



Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) jana wametangaza kumfungulia  msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego pichani juu  kuendelea na shughuli za Sanaa baada ya kuwa ametekeleza adhabu  pamoja na maagizoyote aliyoelekezwa kama masharti ya kumfungulia.

Akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari Katibu Mtendaji  Godfrey Mngereza alisema  BASATA kama mlezi wa wasanii linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe  Nay wa Mitego  kujutia na kukiri kwamba amejifunza na yuko tayari kubadilika na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya.

Hata hivyo, pamoja na kumfungulia kuendelea na shughuli za sanaa baraza linamweka kwenye uangalizi maalum msanii huyo kama sehemu ya kuhakikisha anaendesha shughuli za sanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu sambamba na kuzingatia maadili katika kazi zake.

“Itakumbukwa kwamba  Julai 27 mwaka huu  mwaka huu  Baraza lilimfungia Nay wa Mitego kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo: kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na  kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa,kulipa faini ya Shil.Mil. 1 , kuomba radhi watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, kuufanyia marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’  ili ubebe maudhui yenye maadili” alisema Mngereza. 

Aidha msanii huyo  ametekeleza adhabu zote tajwa hapo juu , pia alikabidhiwa cheti chake cha usajili na kibali cha BASATA.

Hata hivyo, pamoja na kuleta marekebisho mara mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’ Baraza bado halijaridhishwa na marekebisho hayo hivyo linaendelea kuufungia wimbo huu hadi hapo litakapojiridhisha umekidhi vigezo vya kimaadili.

Katika kikao na msanii Nay wa Mitego cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa adhabu yake kilichofanyika Agosti 12 mwaka huu   katika ofisi za BASATA ameagizwa kuendelea kuufanyia marekebisho wimbo wake huo kama bado anaona anauhitaji.

Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla kuacha kuucheza wimbo huo hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo. Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa chombo chochote cha habari kitakachokiuka agizo hili.

Aidha, katika kikao hicho cha tathimini ilibainika kwamba  Nay wa Mitego kwa taarifa potofu alizopewa alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo Kasi lililofanyika Julai 30  mwaka huu akiwa katika adhabu. Kwa kosa hili ameandika barua ya kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa waandaaji wa tamasha hili. 

Baraza linatoa wito kwa wasanii kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za sanaa sambamba na kuhakikisha wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa sana.

No comments:

 
 
Blogger Templates