Social Icons

Friday, August 20, 2010

Fahamu siri ya Kida Waziri kukaa kimya miaka 20 nje ya muziki

Na Abdallah Menssah
Kutana na Kida Waziri ambaye ni Mjukuu wa hayati Shaaban Robert , aliyeacha historia katika bendi ya Vijana Jazz .Kwa mashabiki waliokuwa wakiufuatilia muziki wa dansi katika miaka ya kuanzia katikati ya 1980 hadi mwanzoni mwa 1990, sina shaka watakuwa wanamfahamu mwimbaji Kida Waziri.Kida alikuwa mwimbaji pekee wa kike kwenye bendi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Hemedi Maneti ‘Chiriku’ na ambayo ilikuwa imekusanya nyota kadhaa wa kiume wa uimbaji.Baadhi ya nyota hao ni kama vile Eddy Sheggy, Roshi Mselela, Said Hamis ‘Misukosuko’, Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’, Fred Benjamin.Akiwa na Vijana Jazz, Kida mwenye sauti ya kuvutia na inayoweza kumtoa nyoka pangoni alijipatia umaarufu mkubwa kwa kushiriki vilivyo katika vibao kama vile ‘Penzi Haligawanyiki’, ‘Shingo Feni’, pamoja na ‘Mawifi’.Juzi, mwandishi wa makala hii alibahatika kukutana na Kida maeneo ya Mwananyamala Kichangani, Jijini Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo hiyo ikiwa ni baada ya kumsaka kwa kipindi kirefu ambako alianza kwa kusema.“Nilianza muziki tangu nikiwa na umri wa miaka 14, mwishoni mwa miaka ya 70 nchini Kenya, katika bendi ya Jeshi la nchi hiyo, Yellow Wagoners kwa kushawishiwa na mwanamuziki ninayemkumbuka kwa jina moja la Farida.”Aidha, Kida anasema kuwa Farida ni dada yake, rafiki wa karibu wa familia yao aliyekuwa akiimbia bendi hiyo ya Yellow Wagoners na ambaye mara kwa mara alikuwa anapenda kwenda naye kwenye mazoezi yao.Anasema, alipokuwa akihudhuria mazoezi hayo na Farida, alikuwa akifuatisha polepole baadhi ya nyimbo zilizokuwa zikifanyiwa mazoezi, kitendo kilichomfurahisha dada yake huyo na kumfanya amsisitizie kujifunza kuimba.Kadhalika, anasema kuwa siku moja Yellow Wagoners walikuwa katika mazoezi ya kibao cha kukopi cha muziki wa miondoko ya ‘Country’, lakini Farida alikuwa na mafua hivyo akajaribu kumtania kumuomba amsaidie kuimba.
“Kilichotokea hapo ni kuwa niliimba vizuri kiasi cha kuwashangaza wanamuziki wote waliofurahi na kumpongeza ambako kuanzia hapo, wakaniomba kuhudhuria mazoezini bila kukosa na kushiriki baadhi ya maonyesho yao,” anasema Kida.Anasema mwanzoni mwa mwaka 1980, aliondoka Kenya na kurudi nchini ambako mwaka 1985, alifikia Lugalo, jijini Dar es Salaam kwa dada yake aliyekuwa mke wa Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Anaeleza kuwa, akiwa hapo aliweza kuonyesha maajabu kila pale walipotembelea maonyesho ya bendi ya Jeshi hilo, Mwenge Jazz ambako alikuwa akiimba vibao mbalimbali vya kukopi kikiwamo ‘Malaika’.Mwaka huohuo, 1985, alijiunga na bendi ya The Tanzanite ambayo maskani yake yalikuwa ni katika ukumbi wa Simba Grill enzi za Hoteli ya Kilimanjaro inayofahamika sasa kama Kilimanjaro Kempiski.“Nilivyojiunga na Vijana Jazz, ilikua asubuhi ya siku moja ninayoikumbuka kuwa ilikuwa Jumatatu, mwaka 1987, niliingia kwenye ukumbi wa Vijana Hostel, Kinondoni kwa lengo la kunywa supu na kukuta bendi hiyo ikifanya mazoezi,” anasema.Anaendelea alipoingia alitafuta kiti na kukaa mbali kabisa na jukwaani walipokuwa wakifanya mazoezi Vijana Jazz, ambako muda kidogo akaingia Hamza Kalala ‘Mzee wa Madongo’ na mkewe Stella Kalala aliokuwa akifahamiana nao.Anaeleza kuwa, Kalala alifurahi kumuona pale mazoezini kwao kwa sababu naye mara kwa mara alikuwa akitembelea maonyesho yao na bendi yake ya The Tanzanite, ambako alikuwa akimsisitiza kuwatembelea.Kida anaongeza kwa kusema kuwa,kibao kilichokuwa kikifanyiwa mazoezi na Vijana Jazz siku hiyo kilikuwa ni ‘Iam In Love With Mr Dj cha mwanamuziki Yvonne Chaka Chaka, ambako mwimbaji aliyekuwa amepangwa kukiimba ni Eddy Sheggy.“Lakini kibao kile kilionekana kumpa taabu mno Sheggy, hivyo Kalala baada ya kunitambulisha mimi kwa wenzie, alishauri niruhusiwe kupanda jukwaani kuimba kwa sababu alikuwa anafahamu kwamba nawekimudu kwani alishashuhudia mara kadhaa nikikiimba,” anasema.Kitendo cha yeye kuimba kibao hicho ilikuwa ni kama sumaku iliyovuta mioyo ya wanamuziki wote wa Pambamoto waliofurahi kupita alivyotarajia na kumng’ang’ania kumuomba ajiunge nao.Hata hivyo anasikitika kuwa, akiwa na Vijana Jazz aliyodumu nayo hadi mwaka 1990 alipofariki Maneti, hakuweza kuajiriwa ambako katika kipindi chote alikuwa akipewa posho pekee katika kila onyesho la Jumapili.Kama hiyo haitoshi anazungumzia kifo cha hayati Maneti aliyekuwa mchumba wake na kubahatika kuzaa naye mtoto mmoja wa kike Cecilia, kilimempa changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukwepwa na kuogopwa na baadhi ya watu waliokuwa wakiamini ameachiwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.“Sikufarijiwa wala kupewa matumaini mazuri ya kuendesha maisha na mwanangu Cecilia, badala yake nilikuwa nikiimbwa hadi kwenye vigoma vya daku kuwa bwana wangu keshatangulia bado mimi,” anasema Kida.Anasema kuwa, ilifikia wakati alizushiwa kifo na hatimaye hata msichana wake wa kazi alijazwa maneno ya kuwa naye ataambukizwa Ukimwi hivyo akashawishika nakuamua kuacha kazi kwangu na kuondoka.Kida anasema kuwa hata hivyo hawalaumu waliokuwa wakimzushia ana Ukimwi na kumtangazia kifo, kwa sababu midomo ni mali yao, ila anawaasa na kuwataka kuchunguza kabla kuropoka kwani si vema kuombeana mabaya.Anasema kuwa, mwisho wa ubaya ni aibu hasa baada ya ukweli kudhihirika kama ilivyo kwake yeye ambako ni miaka ishirini sasa imekatika tangu kifo cha Maneti, akiwa bado hai na mwenye afya njema kwa ujumla.“Hivi sasa ninajiandaa kurudi tena katika muziki, kwa kufyatua albamu moja niliyoipa jina la ‘Wifi’ na ambayo itakuwa na vibao sita moto wa kuoteambali,” anasema Kida, mama wa familia mwenye watoto watatu anawataja kwa majina kuwa ni Waziri, Cecilia na Samia.Pia vibao vilivyomo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Nimerudi Tena’, ‘All Music Is Music’, ‘Wifi’ pamoja na nyingine tatu ambazo awali zilirekodiwa na Vijana Jazz; ‘Mary Maria’, ‘Penzi Haligawanyiki’ na ‘Shingo Feni’.Anaongeza kuwa, kibao ‘Nimerudi Tena’ amekirekodi jijini Dar es Salaam, kwenye Studio ya Big Times chini ya Mtayarishaji Said Commorien huku vingine vyote vilivyobaki akiwa amevirekodi Arusha kwenye katika Studio iliyo chini ya Mtayarishaji JC Hussein.Kida anasema kuwa, amewakumbuka mno mashabiki na wapenzi wake anaodai anawapenda huku akieleza kuwa, kimya chake hakikuwa na maana kuwa amewatupa bali ni pirikapirika za maisha.Huyo ndiye Kida Waziri aliyezaliwa mwaka Juni 30, mwaka 1964 Jijini Mbeya na mhitimu wa elimu ya msingi aliyoipata katika shule mbalimbali ndani na nje ya nchi, kutokana na shughuli za kikazi za wazazi wake.Mama mzazi wa Kida anaishi jijini Dar es Salaam na Arusha kwa nyakati tofauti ni mtoto wa kwanza wa marehemu Shaaban Robert, Mwanjaa Shaaban Robert hivyo yeye ni mjukuu wa hayati Shaaban Robert.

No comments:

 
 
Blogger Templates