Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akizungumza
na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini
Tanzania Bw. Toshio Nagase kuhusu Japan na Tanzania kushirikiana katika masula
ya TEHAMA . Bw. Toshio Nagase amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora leo jijini Dar
es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akisisitiza jambo alipokutana na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase. Bw. Toshio Nagase
amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhusu namna
Japan na Tanzania zinavyoweza kushirikiana katika masula ya TEHAMA.
Na. Aron Msigwa - Dar es salaam.
Tanzania na Japan
zinatarajia kuanzisha ushirikiano katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwaunganisha wafanyabishara na vijana wanaojihusisha
na masuala ya TEHAMA ili waweze kunufaika na fursa zilizopo katika nchi hizo.
Hayo yamebainishwa
leo jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo
na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini
Tanzania Bw. Toshio Nagase ambaye alimtembelea ofisini kwake kueleza nia ya Shirika lake na nchi ya Japan kutaka
kuwekeza kwenye Sekta ya TEHAMA nchini Tanzania.
Amesema mara baada ya
kukamilika kwa taratibu zote za ushirikiano katika sekta ya TEHAMA vijana na wafanyabishara
wa Tanzania wataweza kushirikiana na vijana na wafanyabiashara kutoka Japan katika
kubadilishana uzoefu na ujuzi katika masuala ya TEHAMA na kuwawezesha kujiajiri
wenyewe au kuajiriwa ndani na nje ya nchi.
Prof. Kamuzora amesema
kuwa Tanzania na Japan kwa muda mrefu
zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo kupitia miradi
ya ushirikiano hususan ujenzi wa
miundombinu na masuala ya Ufundi.
Aidha, amesema kuwa Tanzania imekuwa ni nchi ya kuigwa
duniani na kupigiwa mfano kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma ya kutuma na
kupokea pesa kupitia simu za mkononi na kufanya malipo mbalimbali.
“sisi kama Serikali tunawakaribisha wenzetu wa Japan kuja Tanzania
kushirikiana nasi kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na kuwekeza nchini kwetu ili
wananchi wetu wanufaike na maendeleo ya Sekta hii kama ambavyo wenzetu wamepiga
hatua kwa kuwa na kampuni za vifaa vya TEHAMA kama vile kampuni ya Sony”. Amesema
Prof. Kamuzora.
Amesisitiza kuwa Serikali
ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli imeweka msisitizo
katika uanzishaji na uendelezaji wa viwanda kwa lengo la kukuza ajira miongoni
mwa watanzania na kuongeza kuwa mkakati uliopo ni kuanzisha viwanda vya
kuzalisha vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa kuwa Soko bidhaa hizo lipo.
Ameongeza kuwa
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na JICA imejipanga kuwekeza katika Elimu,Ujuzi
na Stadi kwa vijana ili waweze kutengeneza Program za TEHAMA ambazo
zinahitajika ndani na nje ya nchi hivyo kukuza uchumi miongoni mwa vijana hao.
Kuhusu kuwekeza
katika Elimu katika masuala ya TEHAMA Prof. Kamuzora amesisitiza kuwa hakuna
nchi iliyowahi kuendelea duniani bila kuwa na wabunifu wake wa ndani na kuongeza
kuwa Tanzania sasa inao vijana wenye uwezo wanaofanya vizuri katika Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano.
“Dhana ya kutengeneza
viwanda lazima ihusishe ubunifu wa kutengeneza Programu, hakuna nchi
iliyoendelea bila kuwa na wabunifu wa ndani tunachohitaji sasa ni uwepo wa
vijana ambao wakao tayari ” Amesisitiza Prof. Kamuzora.
Prof. Kamuzora amesema
Tanzania inazo fursa nyingi za kuwawezesha vijana ikiwemo uanzishaji wa viwanda
vidogo na vya kati vya kutengeneza programu za TEHAMA hivyo ushirikiano
ulioonyeshwa na JICA utawezesha viwanda vya
kutengeneza vifaa mbalimbali kuanzishwa kupitia wabunifu waliopo.
“ Tanzania tunao vijana wabunifu wenye uwezo,
kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) wameweza kubuni na kutengeneza
teknolojia mbalimbali kusaidia shughuli
za Kilimo na uhifadhi wa Maliasili hapa nchini” Amesema.
Aidha, amesema Wizara
kwa kushirikiana na JICA inafanya mpango wa kuwakutanisha wafanyabiashara;
wawekezaji; kampuni; sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano
wa Tanzania na Japan ili kubadilishana uzoefu na kuainisha fursa na maeneo ya
kushirikiana kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo na ushirikiano wa nchi hizo
mbili kwenye Nyanja ya TEHAMA.
Kwa upande wake mwakilishi
Mkuu wa JICA nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase akizungumza mara baada ya
kufanyika kwa mazungumzo hayo amesema kuwa Tanzania na Japan kwa miaka mingi zimekuwa
na ushirikiano wa karibu katika masuala mbalimbali.
Ameipongeza Tanzania
kwa kupiga hatua na kufanya vizuri katika matumizi ya TEHAMA kwenye huduma za
fedha kwa njia ya Simu na kubainisha kuwa Japan inayo mengi ya kujifunza
kupitia mafanikio haya.
Amesma JICA
imejipanga kusaidia awamu ya pili ya program zao nchini Tanzania hususan kwenye
Miundombinu, uwekezaji kwenye TEHAMA na masuala ya kiufundi katika maeneo
mbalimbali ambayo miradi ya ushirikiano inatekelezwa.
Nagase ameeleza kuwa
Japan imejipanga kushirikiana kikamilifu katika masuala ya TEHAMA hususan
kuwawezesha vijana na wafanyabiashara wa Tanzania na Japan kubadilishana
uzoefu, ujuzi, ufundi katika masuala ya TEHAMA.
Amebainisha kuwa
Japan iko tayari kushirikiana na Sekta binafsi nchini Tanzania kupitia biashara
na uwekezaji kwenye makampuni yanayojishughulisha na TEHAMA.
0 Comments