ILANI YA UCHAGUZI YA MTANDAO WA WANAWAKE NA KATIBA NA UCHAGUZI
UCHAGUZI MKUU 2015
Kaimu Mkurugenzi wa TAMWA Edda Sanga akiongea kuhusu ilani ya Mtandao wa wanawake wa katiba na uchaguzi iliyozinduliwa hapo jana katika viwanja vya TGNP Mabibo, Dar es salaam. Wanaofuata ni Mwakilishi wa TAWLA, Mkurugenzi wa TGNP Lilian Liundi na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) Asseny Muro.
UTANGULIZI
Uchaguzi wa mwaka 2015 ni wa kihistoria katika harakati za ukombozi wa mwanamke nchini Tanzania. Mwaka huu tunatimiza miaka 20 tangu serikali wanachama wa Umoja wa Mataifa zikubaliane kuwa na ”Mpango Kazi’’ wa Kumkomboa Mwanamke ujulikanao kama Mpango Kazi wa Beijing (Beijing Platform of Action) ambapo Mtanzania GetrudeI.Mongela alikuwa Katibu Mkuu. Mpango huu uliainisha masuala 12 ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na ushiriki wa wanawake katika ngazi zote za uongozi, uwezeshaji wa kiuchumi, uwezeshaji kisheria, haki za afya ya uzazi, haki za mtoto wa kike na uondoaji wa mila potofu. Miaka 20 ya Beijing,
wanawake wa Tanzania tuko wapi katika nyanja ya siasa na uongozi? Tunaelekea wapi ? Ndio maana tunataka agenda ya uwezeshaji wa wanawake iwe kipaumbele kitakachozingatiwa katika uchaguzi Mkuu 2015. Pia ni mwendelezo wa harakati zetu za kudai mabadiliko ya Katiba Mpya ambapo madai 12 ya wanawake yaliwasilishwa.
Wandaaji wa Ilani hii
Maoni yaliyoko katika Ilani hii yanatokana na mawazo ya taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na haki za wanawake na watoto wa kike chini ya uratibu wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi Tanzania na TGNP Mtandao.
Wanawake na Wanaume wa Tanzania wanaothamini na kupigania Haki za Wanawake na Usawa wa Jinsia tunatoa Ilani hii ya uchaguzi inayobeba rai ya wanawake na wanaume wa Tanzania kwa wagombea na vyama vyao.
Ilani hii Ina malengo gani?
Lengo kuu la ilani hii ni kutoa sauti za pamoja za wanawake na makundi mbalimbali yanayotetea haki za wanawake na watoto wa kike kuhusu ushiriki kamilifu wa wa wanawake katika mchakato mzima wa uchaguzi na kuhakikisha agenda yao inapewa kipaumbele katika mipango ya serikali inayopewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Hali Halisi ya Ushiriki wa Wanawake Katika nafasi za kuchaguliwa
. Wanawake ni wadau muhimu katika shughuli zote za kisiasa, uongozi na maendeleo ya jamii zote hapa nchini. Idadi yao kama wapiga kura, wanachama wa vyama vya siasa na kama wazalishaji wanaoendeleza kizazi ni kubwa na haiwezi kupuuzwa. Pamoja na uhalisia huu inasikitisha kwamba idadi ya Wanawake walioko kwenye uongozi ni ndogo ukilinganisha na idadi yao katika Jamii kwa mfano, katika chaguzi mbili za mwaka 2005 na 2010, idadi ya Wanawake walioteuliwa na vyama vya siasa kugombea haikuwa kubwa kama ilivyo kwa wanaume kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini.
Uteuzi wa Wagombea Ubunge Ndani ya Vyama
Na
|
Uchaguzi 2005
|
Uchaguzi 2010
| |||||
1.
|
Chama
|
Me
|
Ke
|
%ke
|
Me
|
Ke
|
%ke
|
2.
|
CCM
|
213
|
19
|
18
|
215
|
24
|
10
|
3.
|
CHADEMA
|
133
|
11
|
8
|
154
|
25
|
14
|
4.
|
CUF
|
200
|
13
|
6
|
168
|
14
|
8
|
5.
|
NCCR
|
63
|
8
|
11
|
52
|
15
|
22
|
Jedwali linaonesha kwamba hakuna hata chama kimoja ambacho kimefikia walau 30% ya uteuzi wa wagombea wanawake kwenye nafasi ya ubunge.(chanzo:TGNP Contextual analysis 2012)
Ilani hii inaongozwa na Misingi ifuatayo
Kutokana na hali ya usawa wa Kijinsia ilivyo katika nafasi za uongozi , tunataka madai yetu ya kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi na hasa katika kuchaguliwa kushika nafasi za uongozi, yaongozwe na misingi mkikuu ifauatayo:
- Tamko la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR:1948)
- Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979, Articles 7: a, b na c)
- Mpango Kazi wa Beijing (1995)
- Mkataba wa Ziada wa Maputo
Madai ya wanawake
Kutokana na idadi yao kubwa wanawake wana haki ya kujenga hoja ya uhalali wao wa kushiriki katika maendeleo ya Taifa. Serikali ina jukumu kubwa la kusawazisha uwanja wa ushindani na hususani kuweka taratibu kwa wagombea wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kufikia na kunufaika na rasilimali ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi. Kwa mantiki hii, sisi wapiga kura wanawake tunadai yafuatayo :-
TAKUKURU
- Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) idhibiti matumizi ya fedha/ rushwa ikiwemo rushwa ya ngono kwenye chaguzi kwa kusimamia sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010.
Tume za Taifa za Uchaguzi (NEC na ZEC)
- Zisimamie kanuni na maadili ya uchaguzi ambazo vyama vya siasa vimeridhia ili kuwa na uchaguzi huru unaozingatia haki na usawa wa jinsia katika ushiriki na matokeo .
- Ziweke taratibu za kuwezesha wananchi, Wanawake kwa wanaume, wenye mahitaji maalum kama wasiiona,wasio sikia, wenye ualbino, wenye ulemavu wa viungo, wanawake wenye uja uzito au watoto wadogo, na hata wazee wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kama wapiga kura na kama wagombea uongozi katika nyadhifa mbalimbali.
- Zipige marufuku matumizi ya lugha ya kashfa zote hasa zenye kudhalilisha wagombea wa kike/ wenye ulemavu na changamoto nyingine
- Kuimarisha mfumo wa uwajibikaji kwa watendaji hususani taasisi na vyombo vya sheria, vya kulinda haki za wanawake, na zinazohusika na uhamasishaji na elimu ya umma kuhusu haki za wanawake
Jeshi la Polisi
- Jeshi la Polisi au chombo kingine cha ulinzi na usalama kisitumike au kuingilia kwa namna yoyote mchakato wa uchaguzi na kuvuruga amani au kuminya demokrasia kwa sababu uvunjivu wa amani utaathiri zaidi wanawake, wenye ulemavu na watoto
Madai kwa serikali itakayoingia madarakani
- Iweke kipaumbele upatikanaji wa Katiba mpya itakayobeba misingi ya haki za wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni ili waweze kupata haki sawa za uraia, siasa na uchumi na ustawi wa jamii zitakazolindwa kikatiba
- Iweke mikakati endelevu itakayobatilisha sheria zote za ubaguzi wa jinsia ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mpya zitakazolinda utu wa mwanamke na kukataza mwendelezo wa tabia, taratibu na mila zenye kubagua na kuwakandamiza wanawake na watoto wa kike. Aidha serikali ijenge mkakati maalum utakaoondoa ukatili wa kijinsia ndani ya ndoa, ukeketaji, ndoa za utotoni, rushwa ya ngono, ubakaji na vitendo vingine vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
- Iwe na mikakati endelevu na inayotekelezeka itakayojenga misingi ya usawa wa kijinsia katika ngazi zote za uongozi na maamuzi. Hususan, serikali ichukue hatua madhubuti za kisera na kisheria ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa iwiano sawa katika nyanja zote za uongozi pamoja na katika mihimili mikuu mitatu ya uongozi (Serikali, Bunge, na Mahakama) kwa kuzingatia mikataba mbalimbali ya kimataifa.
- Ijenge mikakati itakayomhakikishia mwanamke haki ya uzazi salama nchini. Iwekeze zaidi katika afya ya uzazi kwa ujumla kwa kutambua mzigo mkubwa anaobebeshwa mwanamke kwa kuendeleza kizazi cha Tanzania na kuashiria kuweka rehani haki yake ya msingi ya kuishi kutokana na changamoto anazokumbana nazo wakati wa kutimiza jukumu hili za uzazi.
- Iweke mikakati na taratibu za kuwezesha wanawake kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki rasilimali za umma pamoja na ardhi, madini, miundombinu na vitu vilivyoko nchi kavu na majini.
- Itambue na kutekeleza haki za wanawake wenye ulemavu kwa kutambua kwamba huathirika maradufu na mfumo dume na mifumo yote kandamizi. Pia ichukue hatua za kisera na kisheria kulinda wanawake wenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili ; kuhakikisha wanafikia huduma za msingi za kukimu maisha kama vile huduma za afya, elimu, hifadhi ya jamii na kutokubaguliwa katika ajira.
- Iweke mikakati endelevu ya kuhakikisha haki sawa kwa wanawake za kufikia huduma za msingi ikiwa ni pamoja na maji, afya, elimu, huduma za hifadhi ya jamii. Hususan kutambua mahitaji maalum ya watoto wa kike, watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine katika jamii.
- Ili madai yaliyotajwa hapo juu yatekelezeke, serikali iweke mikakati na taratibu thabiti na endelevu zitakazowezesha kila sekta kutenga bajeti zake kwa mtazamo wa Kijinsia. Hii iandamane na kujenga uwezo wake wa kufikisha azma hii katika utekelezaji wenye manufaa.
- Iweke utaratibu endelevu wa kutekeleza mikataba yote iliyoridhia kuhusu haki za wanawake, mikataba hii itambulike kwamba ni sheria za nchi ili kuepusha ucheleweshwaji wa kutafsiri au kuruhusu tafsri zinazokinzana na misingi ya mikataba husika.
- Ikakikishe kuwepo kwa sheria ya uuandaji wa mahakama za familia ili kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wanawake kwa wakati unaofaa.
Madai kwa vyama vya siasa
Vyama vya siasa ni mhimili mkubwa wa demokrasia shirikishi na ya ushindani. Vile vile vyama vya siasa ni walinzi waLango Kuu la kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa mujibu wa ibara ya 39 (1)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), ambayo inamtaka kila anayewania uongozi kupendekezwa na chama cha siasa. Hivyo basi, vyama vina uwezo mkubwa wa kuamua ni nani aingie kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na nani atolewe, vile vile nani ashinde.
Wanawake tukiwa wapiga kura na wagombea uongozi tunahitaji kuona Vyama vinavyoomba ridhaa ya uongozi kutoka kwa wananchi vikitekeleza madai yafuatayo :-
- Ilani au ajenda kuu za vyama zitambue na kudhihirisha kinagaubaga masuala muhimu ya kiamendeleo ya wanawake yatakayowapelekea kufikia na kunufaika na sera za nchi kama kufikia huduma za msingi, na pia kuwezesha kushughulikiwa kwa vikwazo mbalimbali vya kijinsia vinavyopelekea kumnyima mwanamke fursa na haki zao kama vile Ukatili wa Kijinsia.
- Vijenge na kutekeleza mikakati thabiti na endelevu ya kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu na kulinda haki zao katika mchakato mzima wa uchaguzi zikiwemo uteuzi, kampeni, kupiga kura na baadaye.
- Iwe marufuku kwa chama chochote kumbagua mwanachama kwa misingi ya jinsi, maumbile, dini, ukabila, kanda, hali au fikra mbadala.
- Kuzingatia kanuni za maadili ya uchaguzi ili kujenga heshima na utu wa wagombea, hasa wanawake, wakati wote wa uchaguzi na kuonyesha nia ya kujenga na kuimarisha amani na umoja wa kitaifa.
- Vyama vya siasa vionyeshe nia ya kweli ya kupambana na ufisadi na rushwa za aina zozote zile ikiwa ni pamoja na rushwa ya ngono.
- Kuweka utaratibu thabiti wa kuwakemea na hata kuwaondoa kwenye kinyang’anyiro wagombea watakaotumia lugha za matusi au udhalilishaji kwa wagombea Wanawake kwa nia ya kuwadhoofisha kisiasa
Madai Kwa Wagombea
Kiongozi au mgombea Mwanamke au mwanamume anayetakiwa ni yule ambaye hatatumia nguvu za fedha kwenye kupata uongozi kwa kuwa hali hii hudhoofisha na kukatisha tamaa harakati zote za kuwakomboa wanawake na jamii iliyoko pembezoni kufikia nafasi za uongozi kama rasilimali ya Taifa. Sifa tunazohitaji kutoka kwa mgombea wa uongozi ni hizi zifuatazo:
- Awe ni mtu mwenye historia na makuzi ya uadilifu, utu, uvumilivu, maono ya kutetea haki za wanyonge wakiwemo wanawake, watu wenye ulemavu, wazee, vijana na watoto.
- Asiwe na historia ya udhalilishaji wa aina yoyote ile ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia kwa wanaake na watoto
- Awe na uelewa mpana na uchambuzi wa kina uliojengeka katika misingi ya usawa wa Kijinsia na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi kwa misingi ya haki kwa wananchi anaowawakilisha
- Awe na uwezo wa kuchambua na kujenga na kutekeleza ajenda inayobeba masuala ya msingi ya kumkomboa mwanamke akiwa kama raia na mwakilishi wake.
- Mgombea yeyote kamwe asitumie nguvu ya fedha kununua kura bali atumie busara na nguvu ya hoja kushawishi wapiga kura wakiwemo wanawake katika ngazi mbalimbali.
- Mgombea yeyote au mpambe au shabiki asitumie lugha ya matusi au kuonyesha ubabe wa kudhalilisha wananchi hasa wanawake kama wapiga kura
HITIMISHO
Ilani hii ya uchaguzi ni tamko la pamoja la Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi kutoka mashirika mbalimbali na mitandao,vikundi vya kijamii zaidi ya 65 chini ya uratibu wa TGNP Mtandao ambapo kwa pamoja tunaamini kwamba, mfumo dume, kama ilivyo mifumo yote kandamizi, hauwezi ukajenga mazingira ya kidemokrasia endelevu, wala hauwezi kupunguza au kuondoa umaskini nchini.
Hali kadhalika ilani inasisitiza kwamba hatima ya nchi yetu, iko mikononi mwa wanawake na wanaume wapiga kura na wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa na ya kimapinduzi katika nchi yetu endapo tutaunganisha nguvu zao na kufanya yafuatayo:
· Wanawake wakiwa wapiga kura wakatae kuuza haki zao.
· Wanawake wakatae kurubuniwa na vyama, viongozi auwatu wenye uchu wa madaraka na tabia ya kudhalilisha wapiga kura wao
· Wapiga kura wakatae kuunga mkono vyama au viongozi watarajiwa wanaokumbatia mfumo dume katika uchaguzi mkuu.
Agenda ya Mwanamke,Turufu ya ushindi 2015!
0 Comments