ASHA BARAKA ALAANI WASANII WA KIKE KUJIANIKA JUKWAANI

MKURUGENZI wa Kampuni ya The African Stars Entertainment Asha Baraka.
NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka, amekemea tabia inayoonekana kumea kwa wasanii wa kike kuonyesha maeneo ya siri hadharani.

Kauli hiyo ya Asha imekuja siku chache baada ya muimbaji Zuwena Mohamed ‘Shilole’ kushutumiwa kwa kuonyesha maungo yake ya siri hadharani katika shoo aliyoifanya nchini Ubelgiji.

“Hii tabia inachefua, hasa kwa wasanii wa kike ambao wanadhani umaarufu ni kuanika nyeti zao nje...tena bila haya, wanatudhalilisha wanawake wenzao wa Kitanzania, wanadhalilisha viongozi wanaotambulika katika ngazi za kimataifa na kuonekana wanawake wa Tanzania hatuna maadili,” alisema Asha.

Aliongeza kuwa yeye kama mkurugenzi pia mmiliki wa bendi ya Twanga Pepeta, amekuwa mstari wa mbele kukemea mavazi ambayo hayana staha kwa wasanii wanapokuwa jukwaani.

“Sijui tuseme huu ni ulimbukeni wa kwenda kufanya shoo katika mataifa ya nje au vipi? Nashindwa kuelewa, kwani wanachohitaji watu ni kupata burudani tu si kuonyeshwa maeneo ambayo kila mmoja anayo,” aliongeza Asha.

Pia amelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kwa kutoa karipio kali kwa Shilole na kupanga kumwita ili akajieleze kabla hawajampa adhabu.

Aidha, wadau mbalimbali wa muziki wa aina mbalimbali, wamelaani kitendo hicho cha Shilole na kwamba endapo hakitachukuliwa hatua kali wanaliona anguko la wasanii wa muziki wa kike hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments