GRAND MALT YAMWEKA HADHARANI MWALI WA LIGI KUU YA ZANZIBAR



 Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),Fimbo Butallah akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akitangaza zawadi kwa Mshindi wa Kwanza wa Ligi Kuu ya Grand Malt Zanzibar 2013/14,katika ukumbi wa Mikutano wa Kilimanjaro House,Masaki jijini Dar es Salaam leo.Kushoto ni Meneja wa Kinywaji cha Grand Malt ambao ndio wadhamini wakuu wa Ligi kuu ya Zanzibar,Consolata Adam.

Na Mwandishi Wetu
WADHAMINI wakuu wa Ligi Kuu ya Zanzibar, kinywaji cha Grand Malt jana walianika rasmi kombe atakalokabidhiwa mshindi hapo kesho, huku kukiwa na maandalizi ya sherehe za ‘kufa mtu’.

Mshindi anayetarajiwa kukabidhiwa kombe hilo ni KMKM ambayo ndiyo imefanikiwa kulitwaa taji hilo msimu huu, huku ikitarajiwa pia kuondoka na kitita cha Sh milioni 10.

Katika hafla fupi ya kulionesha kombe hilo iliyofanyika katika ofisi za Grand Malt, Dar es Salaam, Meneja Masoko wa kinywaji hicho, Fimbo Butallah alisema kwao ni heshima kubwa kudhamini Ligi Kuu ya Zanzibar, ambayo kwa sasa ina ushindani mkubwa.

“Sherehe ya kumkabidhi mshindi taji itafanyika keshokutwa (kesho) katika Uwanja wa Amaan, ambapo kutakuwa na pambano la kufunga ligi kati ya KMKM na Zimamoto,” alisema Butallah.

Kwa mujibu wa Butallahatakabidhiwa taji hilo na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ally Idd, ambapo kutakuwa na shamrashamra za kila aina.

Mbali na kupata kombe na fedha, mshindi atapata pia medali, huku mshindi wa pili akiondoka na Sh milioni 5 na medali ambazo zitatolewa na wadhamini wa ligi hiyo, Grand Malt.

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya kufunga ligi hiyo, Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema, kila kitu kimekamilika na wamejipanga kuwapa burudani ya aina yake wakazi wa Zanzibar.

“Tumeandaa vikundi mbalimbali vitakavyotoa burudani uwanjani tangu saa 7 mchana, ikiwemo vikundi vya sarakasi na ngoma maarufu ya Kidumbati hivyo tunawaomba watu wafike mapema uwanjani ili kuweza kupata burudani hizi.”

Grand Malt wameamua kufanya kjufuru zaidi kwani mchezo huo hautakuwa na kiingilio, ili kutoa fursa kwa wapenzi wote wa soka Zanzibar washuhudie jinsi bingwa mpya anavyokabidhiwa kombe.

Grand Malt ndiyo wadhamini wakuu wa ligi hiyo inayojulikana kama ‘Grand Malt Premier League’ na wameidhamini kwa muda wa miaka mitatu.

Post a Comment

0 Comments